Friday, May 9, 2014
MAADHIMISHO YA SIKU YA NDEGE WAHAMAO DUNIANI TAREHE 10 – 11 MEI 2014.
Do you like this story?
JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA
UTALII
TAARIFA KWA UMMA
MAADHIMISHO YA SIKU YA NDEGE
WAHAMAO DUNIANI
TAREHE 10 – 11 MEI 2014
Maadhimisho ya Siku ya Ndege
Wahamao Duniani ni siku ambayo huadhimishwa kimataifa kila mwaka tarehe
10 na 11 Mei.
Wizara ya Maliasili na Utalii
inawashauri wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Ardhi oevu ambayo ni makazi
na mapito ya ndege wahamao kushirikiana na Serikali katika kuwalinda ndege hao
na kuhifadhi mapito na makazi yao.
Wananchi pia wanakumbushwa kuwa
maeneo ya ardhioevu ndio vyanzo vya maji ambayo yanafaa kwa matumizi ya kila
siku ya binadamu, wanyama na ndege, hivyo maeneo hayo ni vyema yalindwe kwa
manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
Kuna aina nyingi za ndege maji na
wahamao. Aina za ndege hao ni kama vile Heroe mkubwa na mdogo (flamingos) ambao
wanahama kila mwaka kutoka sehemu moja ya dunia kwenda nyingine kutafuta
malisho, maji, kukwepa hali mbaya ya hewa na kupata sehemu salama ya kuzaliana.
Tanzania ni nchi mojawapo yenye
sehemu nyingi ambazo ni salama kwa mazalia ya ndege. Kwa mfano, Ziwa Natron ni
maarufu kwa mazalia ya ndege aitwaye Heroe mdogo. Inakadiriwa kuwa asilimia 80
ya Heroe mdogo kote duniani huzalia katika Ziwa Natron liliko Kaskazini mwa
Tanzania. Ziwa hilo ni kivutio cha utalii kutokana na ndege,
wanyamapori na mandhari ya Ziwa.
Maadhimisho ya Siku ya Ndege
Wahamao Duniani yalianza mwaka 2006 na kuendelea kusherehekewa kila mwaka
mwishoni mwa wiki ya pili ya kila mwezi Mei. Watu duniani kote huitumia
fursa hii kutoa elimu na kufanya matembezi katika sehemu zenye Ndege hawa
kwa ajili ya kusherehekea siku hii. Kwa mwaka huu Wizara ya Maliasili itafanya
maadhimisho hayo Katika Eneo la Ramsar la Ziwa Natron lililopo Mkoani Arusha.
Eneo hili lina umuhimu wa ndege wahamao aina ya Heroe mdogo.
Ujumbe wa mwaka huu wa Siku ya
Ndege Wahamao ni: “Mahali Wanapofikia Ndege Wahamao na Utalii (Destination
Flyways; Migratory Birds and Tourism), “. Tafsiri ya ujumbe huu ni kuwa
nchi, mashirika na watu binafsi wanatakiwa kutunza maeneo wanapolazimika
kufikia ndege wahamao kwa kila mwaka kwa ajili ya uhifadhi endelevu wa ndege
hao pamoja na kusaidia jamii kutambua umuhimu wa ndege hao katika kuvutia
utalii.
Utunzaji wa ndege wahamao ni
sababu mojawapo iliyofanya Tanzania kusaini Mkataba wa Uhifadhi wa Ardhioevu
(Ramsar) mwaka 2000. Ardhioevu, pamoja na maufaa mengine ikiwepo maji, chakula,
kurekebisha hali ya hewa, kusafisha maji machafu na kuzuia mafuriko pia ni
makazi ya wanyamapori wakiwemo ndege wahamao.
Kutokana na Mkataba huo Tanzania
imetenga maeneo ya Ramsar ambayo ni muhimu katika kuhifadhi bioanuwai. Maeneo
ya ardhioevu yaliyotengwa hususani kwa uhifadhi wa ndege ni pamoja na Ardhioevu
zenye umuhimu wa kimataifa kama vile:- Malagarasi-Muyovozi ambayo ni muhimu kwa
uhifadhi wa ndege aina ya Korongo domokiatu (Shoebill stork), na eneo la Ramsar
la Ziwa Natron ambalo ni muhimu katika kuhifadhi ndege aina ya Heroe
mdogo (lesser flamingo).
Serikali imekuwa ikiwajengea
wananchi uwezo wa kuhifadhi na kutumia rasilimali za ardhioevu nchini kwa kutoa
elimu ya uhifadhi katika maeneo yanayozunguka maeneo ya Ramsa. Maeneo hayo
ambayo ni makazi muhimu ya ndege wahamao yanasimamiwa na Sheria ya Kuhifadhi
Mazingira ya mwaka 2004 na ya Kuhifadhi Wanyamapori ya Mwaka 2009.
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
9 Mei 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAADHIMISHO YA SIKU YA NDEGE WAHAMAO DUNIANI TAREHE 10 – 11 MEI 2014.”
Post a Comment