Thursday, May 29, 2014
SHEIKH PONDA AGOMA KWENDA MAHAKAMANI, ACHOSHWA NA TABIA YA KESI YAKE KUAHIRISHWA MARA KWA MARA
Do you like this story?
Kiongozi wa Taasisi ya Jumuiya za
Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, jana aligoma kufikishwa mahakamani kutoka
mahabusu ya Gereza la Mkoa wa Morogoro, akidai kuchoshwa kuhairishwa kwa kesi
yake kila anapofikishwa mahakamani.
Pamoja na kuchelewa kufikishwa
mahakamani, kesi yake iliahirishwa tena hadi Juni 10 baada ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Mary Moyo kusema kuwa jalada bado halijarudishwa kutoka Mahakama Kuu,
Kanda ya Dar es Salaam.
Wakili wa kiongozi huyo, Bathelomeo
Tarimo alilalamikia hali hiyo na kutaka haki itendeke kwa mteja wake.
Akizungumza jana, Msajili wa Mahakama
Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Projest Kahyoza alisema kuwa kukwama kwa faili la
Sheikh Ponda ni kutokana na maombi namba 25 ya mwaka 2014 yanayosubiri
kusikilizwa mahakamani hadi sasa.
Msajili alisema kuwa maombi ya Sheikh
Ponda ya kutaka kuharakisha usomaji wa rufaa ili utolewe uamuzi na kesi hiyo
kumalizika au kuendelea, yatasikilizwa na Jaji Lawrence Kaduri, Juni 16.
Kwa upande wake, Wakili Tarimo alidai
kuahirishwa kwa kesi hiyo kunatokana na kucheleweshwa kusomwa kwa rufani yake
namba 89 ya mwaka 2013 aliyowasilisha Mahakama Kuu Septemba 14 mwaka 2013.
Wakili Tarimo alidai kuwa, rufaa hiyo
inahusu moja ya shtaka linalomkabili Sheikh Ponda lililotokana na uamuzi
uliotolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Alidai kuwa majalada yote yanayohusu
kesi ya Sheikh Ponda yapo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, lakini cha
kushangaza kesi imekuwa ikiahirishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, jambo
ambalo alidai kuwa limeanza kumtia wasiwasi mteja wake.
Upande wa Jamhuri unaowakilishwa na
Wakili Sunday Hyera uliiomba mahakama hiyo kuahirisha kesi na kupanga tarehe
nyingine ya kutajwa wakati jalada halisi la kesi hiyo lililoitishwa na Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, likiendelea kusubiriwa kuletwa kortini
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SHEIKH PONDA AGOMA KWENDA MAHAKAMANI, ACHOSHWA NA TABIA YA KESI YAKE KUAHIRISHWA MARA KWA MARA ”
Post a Comment