Wednesday, May 7, 2014

SITTA AONJA SHUBIRI.




MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, na Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, jana alipata wakati mgumu baada ya kulakiwa na kundi kubwa la watu, wengi wao wakiwa vijana waliokuwa na mabango yaliyobeba ujumbe wa ‘serikali tatu’.

Hali hiyo ilijitokeza kabla na baada ya kufungua matawi mawili ya CCM katika eneo la Sahara jijini hapa, ambapo idadi kubwa ya watu wanaodaiwa ni wafuasi wa vyama vya upinzani, walipaza sauti zao kila mara wakimwonyesha alama ya vidole vitatu, wakiashiria kutaka muungano wa serikali tatu na wengine wakionyesha alama ya vidole viwili inayotumiwa na CHADEMA.
Awali hali hiyo haikuonekana kumshitua kiongozi huyo, lakini ongezeko la watu wakati wa ufunguzi wa matawi hayo, waliokuwa wakipaza sauti zao kutaka maoni ya wananchi waliotaka serikali tatu yaheshimiwe, kulimtikisa kiasi cha kumfanya akatishe hotuba yake mara kwa mara.

Kila mara makundi ya watu hao, hususan vijana, walikuwa wakikatiza hotuba yake kwa kuimba; “Tunataka serikali tatu, tunataka serikali tatu, CCM kwisha, CCM kwisha.”
Baadhi ya vijana wa UVCCM, walionekana kukerwa na hali hiyo, ambapo nao walianza kupaza sauti zao wakimshangilia Waziri Sitta kwa kumuita “Jembe, jembe, jembe, jembe.”

Waziri Sitta, alikuwa amepiga kambi jijini Mwanza kwa siku mbili kukutana na kuzungumza na makundi mbalimbali ya vijana wajasiriamali, na kufungua matawi hayo mawili na kituo cha Thamani ya Utu kilichopo kwenye kituo cha mafuta cha MOIL Sabasaba, Manispaa ya Ilemela jijini hapa.

Sitta, aligusia kidogo suala la katiba, akitaka izibane idara zote za umma na kuwa rafiki wa wananchi, kuliko ilivyo sasa ambapo viongozi wengi wanaonekana kuvimba vichwa wanapokuwa kwenye ofisi zenye viyoyozi.

Akizungumza mara baada ya kufungua tawi la CCM la w
apiga debe stendi ya daladala Sahara, Waziri Sitta alisisitiza umuhimu wa viongozi wa idara zote za serikali wakiwemo maofisa uchumi wa kila halmashauri nchini, kushirikiana na vijana kuwawezesha mbinu na maarifa ya kubuni na kusimamia miradi ya kimaendeleo.

Alisema vijana ndio nguzo muhimu sana katika maendeleo ya taifa, hivyo ni lazima suala hilo litiliwe mkazo kwani Tanzania ilipata uhuru wake kwa ajili ya kuwakomboa wananchi wake kutoka kwenye makucha ya wakoloni, ili wajitawale na kupigania maendeleo yao.

“Nikiwa Waziri wa Afrika Mashariki, nimepanga kuhakikisha vijana wa Mwanza ninawaunganisha na vijana wa Kigali Rwanda, Nairobi Kenya, Kampala Uganda na miji mingine ya Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, ili waweze kujitanua kimaendeleo kupitia miradi yao.

“Kumbukeni hapa Mwanza ndiyo kitovu cha nchi za Maziwa Makuu, kwa hiyo tunahitaji kuona vijana mnajinasua kutoka kwenye lindi la umasikini. Na leo hapa nayakabidhi mashina haya mawili ya CCM niliyoyafungua sh 500,000 kila moja,” alisema Waziri Sitta huku akishangiliwa.

Alisema ziara yake hiyo ililenga kukamilisha ratiba yake ya mwaka 2013 iliyohusu kukutana na kuzungumza na makundi mbalimbali ya wajasiriamali, na kuonya kuwa taifa lolote linalowapuuza vijana lina matatizo makubwa.

0 Responses to “SITTA AONJA SHUBIRI.”

Post a Comment

More to Read