Friday, May 9, 2014
WAALIMU WAPYA WILAYA YA HANDENI TANGA WAANZA KAZI KWA MACHUNGU.
Do you like this story?
WAAJIRIWA
wapya wa fani ya ualimu wa shule za msingi katika Wilaya ya Handeni, Mkoa wa
Tanga wameanza kazi kwa kuonja machungu ya madeni baada ya kutopewa stahili zao
zote kabla ya kuanza kazi na kusambazwa kwenye vituo vyao vya kazi kwenye
maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Wakizungumza
na Thehabari.com kwa masharti ya kutotaja majina yao kwa kuhofia kunyanyaswa na
uongozi wa juu wilayani hapo, walisema kuwa kwa mujibu wa makubaliano na
taratibu walitakiwa kulipwa shilingi 245,000 ikiwa ni malipo ya fedha za
kujikimu kwa siku saba yaani shilingi 35,000 kwa kila siku jambo ambalo
halikufanywa.
Mmoja wa
walimu hao walioanza kazi tangu Aprili Mosi, 2014 alisema walipoanza kazi
walilipwa shilingi 140,000 tu na kuahidiwa kiasi kingine kumaliziwa ndani ya
mwezi huo, ahadi ambayo haijatekelezwa ilhali wao wakiangaika na maisha ya
ugenini fedha hawana na wamepigwa marufuku kufuatilia fedha halmashauri hadi
hapo itakapotangazwa.
Alisema
walitegemea kwa kuwa malipo ya kujikimu hawakupewa yote wangelipewa mshahara wa
mwezi Aprili jambo ambalo nalo halikutekelezwa kwani wamejibiwa kuwa, eti
hakuna fedha kwa sasa hadi hapo watakapojulishwa kwenye vituo vyao vya kazi.
"...Wakati
tunaanza kazi (Aprili Mosi) tulipewa shilingi 140,000 badala ya Shilingi
245,000/- tuliahidiwa tungelipwa malipo yaliobaki ndani ya mwezi wa nne lakini
hadi leo hatujalipwa na tumezuiwa kwenda kufuatilia wala kuulizia malipo,
wametuma ujumbe toka halmashauri kwa walimu wakuu kuwa tusiende kufuatilia
mshahara wa mwezi wa nne hadi hapo itakapotangazwa, jaribu kufikiria tunaishi
vipi ugenini?," alisema mmoja wa walimu hao.
Aidha mmoja
wa walimu hao alisema hali ya maisha walipopelekwa ni ngumu ilhali wakitakiwa
kununua vitu vya msingi vya kuanzia maisha kama vile godoro, kitanda, vyombo
vidogo vya ndani na vinginevyo jambo ambalo wengine walifanya na kuishiwa
kabisa na fedha kidunju waliopewa.
"Ndugu
mwandishi hebu wewe fikiria unawezaje kuishi ugenini kwa shilingi 140,000/-
hujanunua godoro, kitanda na maji ndoo moja huku tunanunua shilingi 500, vyombo
vya ndani huna unaishi vipi katika hali kama hii?," alisema mmoja wa
walimu hao huku akionesha kusikitika.
Akizungumzia
taarifa hiyo leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya Handeni, Dk. Khalfany Haule
alipopigiwa simu alioneshwa kushangazwa na taarifa hiyo na kudai atawasiliana
na mwandishi wa habari baadaye, lakini alipotafutwa baadaye simu yake ilikuwa
imezimwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAALIMU WAPYA WILAYA YA HANDENI TANGA WAANZA KAZI KWA MACHUNGU.”
Post a Comment