Saturday, June 21, 2014

TUNDU LISSU AIUMBUA SERIKALI BUNGENI, ADAI IMEJAA UONGO.




Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), amelitaka Bunge la Tanzania kuiwajibisha serikali kutokana na kuwadanganya wananchi.

Akichangia bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15 bungeni jana, Lissu aliituhumu serikali kutoa takwimu za uongo ambazo hazionyeshi hali halisi ya mambo yakiwamo mapato ya serikali huku akilisisitiza Bunge kutimiza wajibu wake kwa kuiwajibisha.

Lissu aliituhumu Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Nishati na Madini kwa kutoa takwimu za uongo bungeni kuhusu fedha za zilizotokana na fidia ya ununuzi wa rada (chenji ya rada) na mapato yatokanayo na mauzo ya madini.

"Jukumu la wabunge si kuisifia Serikali, bali kuisimamia. Na katika kutekeleza wajibu wao huo, wabunge wanapaswa kuihoji Serikali, huo ndiyo wajibu wao kikatiba. Kuna ishara ambazo kwa maoni yangu, zinaenda kinyume kabisa cha wajibu wetu tuliopewa na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," alisema Lissu.

"Governments lie and our government lies' (Serikali huwa zinadanganya na Serikali yetu huwa inadanganya). Mheshimiwa Spika, leo (jana) asubuhi Bunge lako tukufu limeambiwa kuwa madawati ya pesa za chenji ya rada yamegawanywa. Madawati ya platiski ngumu 30,240 kwa halmshauri mbalimbali nchini na madawati ya chuma 63,500," alisema.

Akijibu swali la Mbunge wa Ukonga (CCM), Eugen Mwaiposa, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, (TAMISEMI – Elimu), Kassim Majaliwa, alisema kuwa 2010-13 Serikali ilitenga Sh. bilioni 12.4 zilizotokana na na chenji ya rada kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati katika shule za msingi nchini.

Lakini Lissu alipinga takwimu za Serikali kuhusu idadi ya madawati yaliyosambazwa katika halmashauri mbalimbali kutokana na fedha hizo, akisema ni za uongo.

"Tumeambiwa jumla ya madawati 93,740 yaliyogawanywa kutokana na chenji ya rada, imeandikiwa na ipo kwenye takwimu za Waziri Mkuu, za Serikali, halafu anakuja waziri mdogo, anasema kwamba hatujagawa yote," alisema Lissu.

"Kama hamjagawa yote, kwa nini mnaandika kwamba mmegawanya yote. Kwa hiyo, mnatudanganya. Kwa nini mnadanganya wabunge, mnadanganya Watanzania? Kwani ni ngumu kiasi gani kusema kwamba tutayagawa?" alihoji.

Aliendelea kueleza kuwa katika mgawo huo wa madawati aliouita 'mgawo hewa', mkoa wa Singida anaotoka haujapewa madawati 3,048 ya chuma na plastiki ngumu kama ilivyoelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

"Katika huo mgawo hewa, tumeambiwa kila halmashauri ya mkoa wangu wa Singida ikiwamo halmashauri yangu ya wilaya ya Ikungi imepewa madawati 508. Jana (juzi) sikuwa hapa bungeni, nilikwenda kwenye halmashauri yangu, hakuna hata dawati moja lililopelekwa," alisema.

"Na mchungaji hapa Peter Msigwa (Mbunge wa Iringa Mjini-Chadema) anasema Manispaa ya Iringa hakuna hata dawati moja lililopelekwa wakati imeandikwa madawati 508 yamepelekwa. Mnatudanganya ili iweje?

"Tunataka tuambiwe ukweli mheshimiwa Spika. Na waheshimiwa wabunge kweli mko hapa kutimiza wajibu wenu au kutimiza maslahi yenu tu. Hebu hojini halmashauri zenu zimepelekewa hayo madawati tisini na tatu elfu yanayozungumzwa humu au ni maneno tu mnapigapiga makofi. Serikali inatangaza, tunatakiwa tuisimamie, tunatakiwa tuihoji, tunatakiwa tuiwajibishe," alisema Lissu.

AMVAA MUHONGO
Pia, Lissu aliituhumu Wizara ya Nishati na Madini kutoeleza ukweli juu ya mapato halisi ambayo Taifa linayapata kutokana na madini.

Alisema kuwa katika hotuba ya bajeti iliyowasilishwa wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salumu, kuna takwimu nyingi zinaonyesha kuwa nchi haina matatizo yoyote ya kiuchumi ilhali Watanzania walio wengi wana hali mbaya kiuchumi.

"Kwenye hotuba ya bajeti ya mwaka huu, utadhani nchi hii hakuna shida, nchi hii mambo mazuri, nchi hii maendeleo yapo, hela zipo na kila kitu sawa. Lakini tunajua na Mungu anajua ni uongo, ni maneno tu," alisema Lissu na kuongeza:
"Tumeambiwa kwenye kitabu hiki cha Hali ya Uchumi kwamba mwaka huu wa 2013/14 tumeuza nchi za nje bidhaa mbalimbali na huduma zaidi ya dola milioni 3,700, Sh. bilioni 4,986 mheshimiwa Spika."

Alisema takwimu za Serikali (kitabu cha Hali ya Uchumi 2013/14) zinakinzana na takwimu zilizotolewa na Waziri wa Niashati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/15.

"Tumeambiwa katika kipindi hicho hicho cha mwaka 2013/14 mauzo ya madini nchi za nje, kwa takwimu ya Serikali kwa mujibu wa Hali ya Uchumi mwaka huu ni Sh. bilioni 1.790. Kwa hotuba ya waziri, hapo sasa, anasema ni dola bilioni 1.861.

"Ukisikiliza takwimu hizi mheshimiwa Spika utadhani kwamba hizo ni hela ni za kwetu. Hizo hela ni za hawa wanaomiliki migodi na sisi hatumiliki migodi," alisema.

Akinukuu takwimu za Wizara ya Nishati na Madini huku akionyesha kitabu cha hotuba ya Prof. Muhongo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2014/15, Lissu alisema katika mwaka 2013/14 mapato ya Serikali kutokana na madini yalikuwa Sh. bilioni 189.

"Ukitazama kitabu hiki cha Muhongo, mapato ya Serikali kutokana na madini ni Sh. bilioni 189, kodi mbalimbali au dola milioni 115 kwa wastani, mafunzo ni dola bilioni 1.8 mapato ya Serikali ni milioni 114, haifiki hata asilimia 10 ya mauzo," alisema Lissu na kuongeza:

"Sasa ukitumia takwimu ambazo Serikali inatupa kuhusu mambo mazuri, madini ya mabilioni mengi yanauzwa, utafikiri ni hela zetu, kumbuka hizo fedha si zetu, ni za wawekezaji."

"Tumetunga sheria za madini na tumetunga sheria za uwekezaji zinazosema kwamba hawa ndiyo tuwakabidhi madini na sasa tunawakabidhi gesi waimiliki," alisema Lissu.

KAMATI YA BAJETI YALIPULIWA
Wakati Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge imetajwa kulipwa posho za kutisha kwa siku, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, ameitupia kombora jingine baada ya kuhoji sababu za wajumbe wake kutohudhuria kikao cha Bunge hilo jana asubuhi.

Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali juzi alitoboa siri Bungeni kwamba kila mjumbe wa kamati hiyo analipwa Sh. 500,000 wanapokuwa katika kikao.

Mpina alisema wajumbe kamati hiyo hawatendi haki kwa kutohudhuria vikao vya Bunge la bajeti kwa vile kamati hiyo ni muhimu katika upitishaji wa bajeti hiyo.

"Tunajadili bajeti, lakini wajumbe wa Kamati ya Bajeti hawamo humu bungeni, wako kwenye vikao vyao. Tunapangaje ratiba za namna hii mheshimiwa Spika? alihoji.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, hakujibu hakusema chochote juu ya utoro wa wajumbe hao jana mchana.

Aidha, Mpina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, aliitaka Serikali kuweka wazi taasisi na watu waliotumia Sh. trilioni 9.36 zilizoongozeka katika Deni la Taifa ndani ya miezi tisa.

"Deni la Taifa ndani ya miezi tisa tu limeongezeka kwa Sh. trilioni 9.36 na inaelezwa kwamba sababu za kuongezeka ni mikopo mipya na kulipa madeni mengine. Tunataka, kabla ya kuunga mkono hoja tuambie fedha hizo zilienda kwenye wizara gani," alisema Mpina.

Mpina pia alikosoa matumizi ya dola ili kulinda ushindani wa Shilingi ya Tanzania akisema kuwa Serikali imeyaruhusu bila sababu za msingi.

0 Responses to “TUNDU LISSU AIUMBUA SERIKALI BUNGENI, ADAI IMEJAA UONGO.”

Post a Comment

More to Read