Saturday, June 21, 2014

WANAFUNZI 39,000 VYUO VIKUU WAOMBA MIKOPO.



IKIWA zimebaki siku 10 kufungwa kwa shughuli ya kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2014/2015, takribani wanafunzi 39,000 wameshatuma maombi yao kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Akizungumza jana kwenye maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano (HESLB), Cosmas Mwaisobwa alisema idadi hiyo ni kwa wanafunzi wapya pekee.

HESLB ilifungua dirisha la kutuma maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2014, Aprili mwaka huu na maombi hayo yamekuwa yakifanywa kwa njia ya mtandao (OLAS) na yatafungwa Juni 30.

Serikali imetenga kiasi cha Sh bilioni 306 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 98,000 wa vyuo vya elimu ya juu nchini, ikiwa wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo.

“Wanafunzi wanaotaka kutuma maombi yao ni vyema wakatumia muda huu uliobaki, kwani Bodi haitatoa muda wa nyongeza kwa watakaochelewa kutuma maombi yao,” alisema.

Akizungumzia hatua ya Bodi kufungua ofisi ya Kanda ya Ziwa, mkoani Mwanza, Mwaisobwa alisema hii ni katika kutekeleza mikakati ya Bodi katika kusogeza huduma karibu na wananchi.

“Mpango mkakati wetu wa miaka mitano kuanzia mwaka 2010, ilikuwa ni kufungua ofisi za kanda katika kuongeza ufanisi katika kuwahudumia na kusogeza huduma kwa wananchi, na mpaka sasa tumefungua ofisi za kanda tatu.”

Mbali na ofisi ya Mwanza itakayohudumia mikoa sita ya Simuyu, Geita, Shinyanga, Kagera, Mara na Mwanza yenye, pia Bodi ina ofisi katika Kanda ya Kati yenye ofisi Dodoma na Zanzibar.

Alisema ofisi ya Mwanza itakuwa inafanya majukumu yote ikiwamo ya utoaji mikopo kwa wanafunzi wenye sifa waliodahiliwa na urejeshwaji wa mikopo kwa wanufaika wa mikopo hiyo.

“ Ofisi hii itasaidia sana wananchi ambao walikuwa wakilazimika kutumia siku nyingi kufika ofisi zetu Dar es Salaam kupata huduma, lakini sasa watahudumiwa huko huko,” alisema.

0 Responses to “WANAFUNZI 39,000 VYUO VIKUU WAOMBA MIKOPO.”

Post a Comment

More to Read