Saturday, July 19, 2014
WANANCHI WATAKIWA KUWATUMIA WASAIDIZI WA KISHERIA KUTATUA MIGOGORO.
Do you like this story?
Serikali
imewataka wananchi kuwatumia wasaidizi wa kisheria (paralegals) katika kutatua
migogoro mbalimbali ya kisheria wanayokabiliana nayo na kuepuka kupeleka
mahakamani migogoro ambayo inaweza kusuluhishwa nje ya Mahakama.
Wasaidizi wa
kisheria ni watu ambao hawana sifa za kuwa mawakili lakini kutokana na uzoefu
na ujuzi wao wanaweza kufanya kazi za usaidizi wa kisheria na hivyo kushiriki
katika kutatua migogogoro mbalimbali katika jamii.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam leo (Ijumaa, Julai 18, 2014), Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mheshimiwa Angellah Jamsine Kairuki amesema kwa kufanya hivyo, wananchi
watakuwa wanashiriki moja kwa moja katika kupunguza mlundikano wa mashauri
mahakamani.
“Nichukue
fursa hii kuwasihi wananchi wanaokabiliwa na migogoro mbalimbali kuwatumia vyema
wasaidizi wa kisheria katika utatuzi wa migogoro,” amesema Naibu Waziri Kairuki
katika mkutano wake wa majumuisho ya ziara ya siku tano jijini Dar es Salaam
ambapo alizitembelea taasisi 13 zinazotoa huduma za msaada wa kisheria kwa
wananchi wasio na uwezo.
Taasisi hizo
alizotembelea Naibu Waziri Kairuki ni pamoja na Chama cha Wanasheria cha
Tanganyika (TLS), Envirocare, Kamati ya Msaada wa Kisheria ya Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM-LAC), Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania
(LST), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Kituo cha Msaada wa
Kisheria kwa Wanawake (WLAC).
Taasisi
nyingine zilizotembelewa ni Kituo kinachoshughulikia Maslahi ya Wanawake na
Watoto (TWCWC), Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wajane na Watoto (CWCA), Chama
cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Chuo
Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Nyumba ya Amani na Ofisi ya Mfuko wa Huduma za
Kisheria (LAF).
Mafanikio na
changamoto
Katika
mkutano huo, Naibu Waziri Kairuki amesema ameshuhudia mafanikio mengi katika
ziara yake yakiwemo kuanzishwa kwa kada ya wasaidizi wa kisheria ambao
wanawafikia wananchi wengi kwa ukaribu katika maeneo yao na kuwapa msaada wa
kisheria.
“Wasadizi
hawa wameweza kutatua migogoro mingi katika jamii zetu bila kufikisha nashauri
mahakamani na hivyo kupunguza uwezekano wa mlundikano wa mashauri mahakamani,’
amesema.
Ametaja
mafanikio mengine aliyokutana nayo kuwa ni pamoja na asasi hizo kushiriki
katika mapambano dhidi ya ukimwi, ukatili wa kijinsia na kingono pamoja na
baadhi ya taasisi kuanza kutumia huduma za kisasa katika kutoa huduma zikiwemo
simu za mkononi.
“Baadhi ya
taasisi kama TAWLA wanatoa huduma kupitia namba0800751010 (Vodacom)
na namba 110017 (TTCL) wakati WLA wanatoa huduma kupitia namba 0800780100 ….hii ni kazi nzuri,” amesema.
Kuhusu
changamoto alizokutana nazo katika ziara yake, Naibu Waziri Kairuki amesema
amepokea malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi mahakamani na malalamiko ya rushwa
katika vyombo vinavyojihusisha na utoaji wa haki. Changamoto nyingine ni pamoja
na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu nafasi ya wasaidizi wa kisheria katika
utatuzi wa migogoro.
Chombo cha
mpito (LAS)
kuratibu
utoaji msaada wa kisheria
Kwa mujibu wa
Naibu Waziri Kairuki, kutokana na mchango mkubwa wa taasisi zinazotoa msaada wa
kisheria kwa wananchi, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeunda
chombo cha mpito kinachoratibu shughuli ya utoaji huduma za msaada wa kisheria
nchini kinachofahamika kama Sekretariaeti ya Msaada wa Kisheria (Legal Aid
Secretariat).
“Kupitia
sekretarieti hii, wadau wanaotoa msaada wa kisheria wanapata ruzuku kutoka
Serikalini ili kuweza kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na
uwezo,” amesema Naibu Waziri Kairuki katika mkutano uliohudhuriwa pia na
Wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti hiyo wakiwemo Dkt. Hellen Kijo-Bisimba, Bi.
Theodosia Muhulo na Bw. Gideon Mandes.
Naibu Waziri
ameongeza kuwa tangu Sekretarieti hiyo iundwe mwezi Agosti, 2012 hadi mwishoni
mwaka wa fedha uliopita (Juni, 2014), Serikali na wadau wa maendeleo walikuwa
wametoa zaidi ya Tshs 1.55 bilioni kwa taasisi 20 zinazotoa huduma za msaada wa
kisheria nchini.
“Na kimsingi
asilimia 97 ya fedha za kuendesha LAS zinatolewa na Serikali na asilimia tatu
inatoka kwa wafadhili,” amefafanua Naibu Waziri Kairuki ambaye ni mwanasheria
kitaaluma na kuongeza kuwa kutokana na uwezeshaji huo, mafanikio kadhaa
yamepatikana kama alivyoshuhudia katika ziara yake.
Kairuki
ameongeza kuwa kupitia fedha hizi, Sekretarieti imeweza kuwafikia na kutambua
walipo watoa huduma za msaada wa kisheria na kuanzisha kanzidata
(database) inayoonyesha hudua wanazotoa na mahali walipo.
“Hii ni hatua
kubwa sana ikizangatiwa kuwa awali taasisi hizo zilitoa huduma bila kutambuliwa
au kutambuana jambo lililowanyima fursa ya kubadilishana uzoefu na kushirikiana
katika kutekeleza majukumu yao,” amsema.
Akiongea
katika mkutano huo, Kwa upande wake, Bi. Muhulo ambaye pia ni Mkurugenzi wa
WLAC ameipongeza ziara ya Naibu Waziri na kusema imeboresha mahusiano baina ya
watoa huduma za msaada wa kisheria na Seriali na kusisitiza ushirikiano huo ni
muhimu katika utoaji wa huduma bora za kisheria.
Kwa upande
wake, Dkt. Kijo-Bisimba ambaye pia ni Mkurugenzi wa LHRC amesema taasisi
zinazotoa msaada wa kisheria kwa wananchi zimefurahishwa na hatua ya Naibu
Waziri Kairuki kuzitembelea, kukutana na watumishi na wananchi wanaopata msaada
wa kisheria badala ya kusikia huduma hizo kupiti vyombo vya habari.
“Tumefurahishwa
sana na kututembelea…wengine wanasikia tu kutoka kwenye vyombo vya habari
lakini yeye ametembelea hadi sehemu tunazotoa huduma za msaada,” amesema Dkt.
Kijo-Bisimba na kushauri kuwa wakati umefika kwa kutungwa kwa sheria
itakayowatambua wasaidizi wa kisheria na kuratibu utendaji wao kwa manufaa ya
wananchi.
Akizungumza
katika mkutano huo uliofanyika katika Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria, Bw.
Mandes ambaye pia Wakili wa Kujitegemea ameishukuru Serikali kwa kuonyesha
utayari wa kutunga sheria itakayoratibu wasaidizi wa kisheria (paralegals) na
kushauri kuongezwa kwa kasi ili sheria hiyo ipatikane haraka.
Akifafanua
kuhusu utungwaji wa sheria itakayoratibu wasaidizi wa sheria, Naibu Waziri
amesema maandalizi ya kutungwa kwa sheria hiyo yamefikia hatua nzuri Serikalini
kabla ya kupelekwa bungeni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WANANCHI WATAKIWA KUWATUMIA WASAIDIZI WA KISHERIA KUTATUA MIGOGORO.”
Post a Comment