Saturday, July 19, 2014

WACHINJA NYAMA MJINI KIBAHA MKOANI PWANI WAGOMA.




Na John Gagarini, Kibaha

SAKATA la Umoja wa wafanyabiashara wa nyama na mazao yake  wilayani Kibaha mkoani Pwani (UWABINK) leo umechukua sura mpya  baada ya kufanya mgomo wa kutochinja ngombe na kusababisha nyama kukosekana kwenye mji wa Kibaha na vitongoji vyake.

Kutokana na mgomo huo wa kutochinja ngombe kumesababisha nyama kukosekana katika maeneo ya kuanzia Maili Moja hadi Visiga na Kibamba CCM wilaya ya Kinondoni Jijijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa umoja huo Athumani Mkanga alisema kuwa wameanza mgomo huo kwa muda usiojulikana kutokana na Halmashauri hiyo kuwahamisha kutoka katika machinjio ya Maili Moja na kuwahamishia machinjio mpya ya Mtakuja kata ya Pangani jirani hifadhi ya msitu wa Ruvu.

Mkanga alisema kuwa hawakatai kuhamia katika machinjio hayo mpya lakini wanashindwa kufanya hivyo kutokana na mapungufu yaliyopo hususani miundombinu kutokuwa rafiki kiusalama , kutokuwa na umeme unaolingana na kazi yao na maji.

“Katika machinjio ya awali walikuwa wakigharamia maji kwa sh 30,000 kwa siku ambapo kwasasa watatakiwa kugharamia maji kutoka Maili Moja kwa sh 150,000 ambayo kwa mwezi ni zaidi ya sh mil 4,” alisema MKanga.

Kwa upande wa mfanyabiashara wa nyama Maliseli Boniface alisema machinjio hayo mapya haijakidhi mahitaji wakihofia kupoteza mali zao kutokana na machinjio hiyo kuwa umbali wa km zaidi ya 5 kutoka Maili Moja na wafanyabiashara hao wakitakiwa kufuata nyama nyakati za alfajiri kukiwa giza huku eneo hilo likiwa limezungukwa na msitu.

“Machinjio hiyo mpya ni ndogo ukilinganisha na ile ya awali kwani ilikuwa ikichinja ng’ombe 35 -40 kwa siku na kwasasa wanaotakiwa kuhamia watakuwa wakichinja ng’ombe 15-20 jambo ambalo itazorotesha biashara hiyo,” alisema Boniface.

Aidha msimamo wa wafanyabishara hao ni kuhamia Machinjio ya Mlanizi kama halmashauri hiyo ikiendelea na msimamo wa kuwahamishia katika machinjio ambayo haijakamilika kimiundombinu .

Akizungumzia mgomo huo Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha Jennifer Omolo  alisema kuwa  hana taarifa kuhusiana na mgomo huo .

Omolo alibainisha kuwa bado anasimamia agizo lake la kuwataka wafanyabiashara hao kusitisha mgomo huo na kuwa machinjio ya Maili Moja isitumike kuanzia julai 18 na badala yake itumike machinjio mpya ya Mtakuja ambayo imekamilika  .

Kutokana na mgomo huo umeathiri kwa kiasi kikubwa walaji kwa kutokuwa na nyama mabucha yote ya maeneo ya kibaha na bucha chache zikiwa zinauza nyamailiyolala(ndaza )kwa sh . 6,000 ambayo ni bei ya nyama ya kawaida.

Hata hivyo halmashauri ya kibaha mji imekuwa ikipokea ushuru wa machinjio ya awali kwa kiasi cha sh. sh. mil 1.6 kwa mwezi ikiwa ni sh.5,000 kwa kichwa kimoja cha ng’ombe hivyo kuhofiwa Halmashauri hiyo kupata hasara ya mapato ya ndani.

0 Responses to “ WACHINJA NYAMA MJINI KIBAHA MKOANI PWANI WAGOMA. ”

Post a Comment

More to Read