Tuesday, July 29, 2014
BABA AWACHARAZA BAKORA WALIMU WAWILI MKOANI TABORA KWA KUMRUDISHA NYUMBANI MTOTO WAKE KUSHONA SARE YA SHULE.
Do you like this story?
Vitendo vya baadhi ya wazazi, kudhalilisha walimu vinaendelea, ambapo mzazi mmoja Selemani Juma, amewashambulia walimu wawili kwa viboko.
Amefanya hivyo kupinga mwanawe
kurudishwa nyumbani, akashone kaptura. Alifanya hivyo mwishoni mwa wiki
iliyopita.
Taarifa zilizomfikia mwandishi
zilibainisha kuwa Juma alidhalilisha walimu wawili wa Shule ya Msingi
Nzogimlole iliyopo wilayani Nzega mkoani Tabora.
Aliwashambulia kwa viboko, akipinga
kitendo cha mwalimu mmojawapo, kumrudisha nyumbani mwanawe.
Mwandishi alifika katika shule hiyo,
yenye walimu tisa tu na kuzungumza na Mwalimu Mkuu Msaidizi, Emmanuel Josephat,
ambaye alisema mwanafunzi huyo, Shaaban Maziku anayesoma darasa la pili,
alipeleka ujumbe tofauti na alioagizwa na walimu kwa baba yake, hivyo
kusababisha kadhia hiyo.
Kwa mujibu wa Mwalimu Josephat, mwalimu
aliyedhalilishwa (jina limehifadhiwa), alikuwa akifundisha katika darasa hilo
na alipomuona mwanafunzi huyo kavaa kaptura iliyochanika vibaya, kiasi cha
sehemu za siri kuonekana, alimrudisha nyumbani kwenda kurekebisha sare yake.
Mwalimu Josephat alisema mwalimu huyo
wa kiume wa darasa la pili, alimwagiza mwanafunzi wake aende kwa baba yake,
akamuombe amsaidie kushona kaptura hiyo.
‘’Mwalimu hana kosa, kwani mtoto
kaptura yake ilikuwa imechanika vibaya kiasi cha sehemu zake za siri
kuonekana… walimu hatupaswi tuwaache hivi watoto, mwalimu alichofanya ni
kumwambia akamwambie baba yake aishone ile sare, lakini mambo hayakuwa hivyo,’’ alisema Mwalimu
Josephat.
Akizungumza kwa majonzi, Mwalimu
Josephat alisema mtoto huyo alipofika nyumbani, alimweleza baba yake kuwa
mwalimu huyo, amechana kaptura hiyo na amemwagiza arudi nyumbani kwenda
kumwambia baba huyo aishone.
Ujumbe huo unadaiwa kusababisha mzazi
huyo, kufika shuleni na kuanza kutoa lugha chafu dhidi ya mwalimu huyo na
baadaye baba huyo alianza kutoa kipigo.
Mwalimu Josephat alidai kuwa baba huyo,
alianza kutumia mawe kurusha kwa walimu hao. Baadaye alitumia fimbo, kumchapa
mwalimu huyo wa darasa la pili.
Hatua hiyo inadaiwa ilisababisha
mwalimu huyo, kupiga mayowe kuomba msaada. Wananafunzi waliokuwa darasani,
walitoka na kuanza kumsaidia kupiga kelele za kuomba msaada.
Mayowe hayo yalisaidia mwalimu
mwenzake, Elias Kafiku kutoka ofisini kwa nia ya kuamua ugomvi huo ili
wazungumze kiofisi na kufikia muafaka. Lakini, mwalimu huyo pia aliambulia
kipigo.
Kutokana na kipigo hicho, mwalimu huyo
wa darasa la pili alipata majeraha na kupelekwa zahanati ya kijiji, ambako
alipatiwa huduma na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Akizungumza na mwandishi, mwalimu huyo
wa darasa la pili alisema hali yake inaendelea vizuri. Alisema sababu ya
kupigwa na mzazi huyo, hazijui kwa kuwa alitekeleza majukumu yake kama kawaida.
Akitoa maoni yake kuhusu tukio hilo,
Mwalimu Elizabeth Kafulila wa shule hiyo, alisema tukio hilo limewatia hofu
katika utendaji kazi, kutokana na mzazi kuingilia majukumu ya walimu.
Mwalimu Elizabeth aliwataka wazazi
kujirekebisha na kushirikiana na walimu katika kulea watoto wao, na wanapokuwa
na malalamiko, wafuate taratibu za kiofisi.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzan
Kaganda alisema mzazi huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kupiga na
kujeruhi vibaya na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Tukio hilo limekumbushia tukio la mwaka
2009 ambapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Albert Mnali,
aliamuru askari kucharaza bakora walimu wa shule za msingi wa wilaya hiyo.
Mnali anadaiwa aliwaamrisha askari
Polisi kuwacharaza viboko walimu hao, kutokana na kusababisha wanafunzi kufeli
mitihani pamoja na pia kuchelewa kazini.
Walimu walioripotiwa kuchapwa viboko na
Mkuu huyo wa Wilaya ni wa shule za msingi za Katerero, Kanazi na Kasenene
mkoani Kagera.
Walimu karibu nchi nzima, walilaani
kitendo hicho, wakisema kimewadhalilisha na kimekiuka haki za binadamu.
Baadaye, Serikali ilichukua hatua ya
kumstaafisha kazi Mkuu huyo wa Wilaya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BABA AWACHARAZA BAKORA WALIMU WAWILI MKOANI TABORA KWA KUMRUDISHA NYUMBANI MTOTO WAKE KUSHONA SARE YA SHULE.”
Post a Comment