Friday, July 25, 2014

JAJI WA MAHAKAMA KUU AFUNGUA KESI YA MADAI YA SH. MILIONI 300 KUTOKANA NA AJALI ILIYOSABABISHWA NA UZEMBE WA DEREVA.




Jaji wa Mahakama Kuu, Grace Mwakipesile amefungua kesi ya madai ya kulipwa fidia ya Sh milioni 300 kutokana na majeraha na maumivu aliyoyapata katika ajali aliyoipata mkoani Shinyanga.

Amefungua kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya dereva Kamota Hassan, Michael Mosha na kampuni ya bima ya Zanzibar. Kesi hiyo itatajwa Agosti 4 mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa.

Katika hati ya madai, Jaji Grace anaiomba mahakama iamuru walalamikiwa hao wamlipe fedha hizo kutokana na ajali anayodai ilitokana na uzembe wa dereva Hassan aliyekuwa anaendesha gari aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 683 AKN, iliyokuwa imewekewa bima na kampuni ya Zanzibar.

Inadaiwa Septemba 17 mwaka 2011 katika kijiji cha Bubihi, Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, Jaji Grace akiwa abiria kwenye gari aina ya Toyota Landcruiser lenye namba za usajili STJ 1870 likiendeshwa na Mosha, waligongwa na Fuso hilo.

Anadai kutokana na ajali hiyo alipata maumivu na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili na kupelekwa katika hospitali ya mkoa ya Shinyanga ambapo alipata matibabu na kuhamishiwa Taasisi ya Mifupa, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI) ambapo aliendelea na matibabu ya nje kwa miezi sita.

0 Responses to “JAJI WA MAHAKAMA KUU AFUNGUA KESI YA MADAI YA SH. MILIONI 300 KUTOKANA NA AJALI ILIYOSABABISHWA NA UZEMBE WA DEREVA.”

Post a Comment

More to Read