Friday, July 25, 2014

SIMBA, YANGA ZAHUSIKA KUIBOMOA MTIBWA SUGAR KILA MWAKA, MEXIME ALALAMA!


Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime



MTIBWA sugar kila mwaka inabomolewa na timu nyingine za ligi kuu soka Tanzania bara kwa kuwasajili wachezaji wengi muhimu wanaong`ara klabuni hapo.

Kocha mkuu wa klabu hiyo, Mzalendo, Mecky Mexime amesema amejikuta kila mwaka anakuwa na kazi ya kujenga upya timu, kwasababu msimu unapoisha, wachezaji watatu au wanne wa kikosi cha kwanza wananunuliwa na timu nyingine zikiwemo Simba na Yanga.

“Timu nyingi zinaangalia kwetu Mtibwa, kila mwaka tunabomolewa, kila mwaka unajenga upya timu, kwasababu wanaondoka wachezaji watatu wanne, tena wachezaji muhimu”. Alisema Mexime.

“Sisi hatusajili wachezaji wa gharama, tunatafuta vijana wadogo na kuwajenga, lakini unakuta mwakani wamenunuliwa tena”.
Beki huyo na Nahodha wa zamani wa Mtibwa na timu ya taifa ya Tanzania , Taifa Stars alikiri kuwa kutengeneza upya timu ni jambo gumu, lakini amekuwa akijitahidi kila msimu kuja na vijana wapya.

Kuhusu maandalizi ya ligi kuu, Mexime alisema wana siku ya tatu tangu waanze kujifua jijini Dar es salaam, na wanamshukuru Mungu wanaendelea vizuri.

“Namshkuru mwenyezi mungu mazoezi yanakwenda vizuri na ninamuomba mwenyezi mungu awape wachezaji nguvu ili waweze kuyapokeza vizuri mafundisho” . Alisema Mexime.
Pia kocha huyo alisema wakati huu wa maandalizi wanahitaji mechi za kirafiki ili kujipima uwezo wao na Agosti 8 mwaka huu amethibitisha kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Azam fc ndani ya dimba la Taifa jijini Dar es salaam.

Siku za karibuni, Simba ilimsajili mlinda mlango nambo moja wa Mtibwa Sugar, Hussein Sharrif `Casillas`, lakini Mexime alisema kipa huyo hajaondoka na Mtibwa, hivyo watasajili kipa mwingine.

Kwa muda mrefu Mtibwa imekuwa kitalu cha kuzalisha wachezaji wanaochukuliwa na timu za Simba na Yanga, kwa mfano Hussein Javu, Said Bahanuzi waliojiunga na Yanga wakitokea Mtibwa.

Wapo wachezaji wengi waliotokea Mtibwa na kujiunga na timu za Simba na Yanga, kama vile Mussa Hassan Mgosi, Juma Kaseja, hivyo ni kweli kuwa klabu hiyo imekuwa ikibomolewa mara nyingi.

0 Responses to “SIMBA, YANGA ZAHUSIKA KUIBOMOA MTIBWA SUGAR KILA MWAKA, MEXIME ALALAMA!”

Post a Comment

More to Read