Saturday, July 19, 2014
WAZIRI DKT MAHENGE AKATAA KUKIPA KIWANDA CHETI, KISA MAJI YAKE YAMEBABUA WATOTO MIGUU.
Do you like this story?
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Mazingira), Dk Binilith Mahenge amekataa kuwapa cheti cha utunzaji wa
mazingira kiwanda cha nguo cha Nida kilichopo Tabata katika Manispaa ya Ilala,
Dar es Salaam.
Mahenge alisema kampuni hiyo imekosa
vigezo wanavyohitaji kwa kuwa maji yake ya viwandani yanatuhumiwa kusababisha
kubabuka miguu kwa watoto wanaochezea maji ya mto Msimbazi ambao NIDA wanamwagia
maji yao ya kiwandani.
‘’Mlipochunguzwa na Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ilionekana kuwa mmefikia kiwango cha
kupata cheti hicho, lakini nimeona kwa macho yangu kuwa mnaidanganya
Serikali,’’ alisema Mahenge.
Alisema serikali inahitaji wawekezaji
wanaowajali Watanzania na wanaolinda afya zao kwa kutunza mazingira na sio kuwa
chanzo cha madhara kwa jamii.
‘’Imenibidi kujiridhisha na hali halisi
ya eneo kwani nimeona kuwa hali ya mto imekuwa mbaya kwa kuwa kuna maji machafu
yenye rangi tofauti ambayo ni hatari kwa viumbe hai wakati NEMC walinipa
taarifa kuwa tayari mmetimiza vigezo,’’ aliongeza.
Kwa mujibu wa Mahenge, kutokana na hali
hiyo kiwanda hicho kinapaswa kuadhibiwa kwa kudanganya.
Naye Diwani wa Kata ya Kigogo, Richard
Chengula alisema wakazi wa eneo lake wanatumia maji hayo kwa ajili ya
kumwagilia mboga hivyo maji yanayotoka katika kiwanda hicho yanawaathiri sana.
Alisema ni kwa muda mrefu kiwanda hicho
kinafungua maji ambayo yana rangi tofauti na kwamba watoto wanaocheza maeneo
hayo na wakazi wanaathirika kiafya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI DKT MAHENGE AKATAA KUKIPA KIWANDA CHETI, KISA MAJI YAKE YAMEBABUA WATOTO MIGUU.”
Post a Comment