Monday, August 4, 2014
WASIWASI UMEIGHARIMU TAIFA STARS- NOOIJ
Do you like this story?
Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema moja ya
sababu za kikosi chake kupoteza mechi dhidi ya Msumbiji (Mambas) ni wachezaji
wake kucheza kwa wasiwasi katika kipindi cha kwanza.
Taifa Stars iliruhusu bao la kwanza sekunde chache
kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza katika mechi ya marudiano ya raundi ya
pili ya michuano ya Afrika kutafuta tiketi ya kucheza hatua ya makundi
iliyochezwa leo (Agosti 3 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto hapa
Maputo.
Bao hilo katika mechi hiyo iliyomalizika kwa
wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao
4-3 lilifungwa kwa kichwa na mshambuliaji Josemar Machaisse.
Nooij alisema wasiwasi katika kipindi cha kwanza
ndio ulioipa Msumbiji fursa ya kutawala mechi hiyo katika kipindi hicho na
kukimalizia ikiwa mbele kwa bao hilo la mshambuliaji huyo wa klabu ya Bravos de
Maquis ya Angola.
Alisema timu yake ilitulia kipindi cha pili baada
ya kumuingiza Amri Kiemba badala ya Khamis Mcha. Pia alilalamikia bao ambalo
Taifa Stars ilifunga dakika ya 16 kupitia kwa John Bocco lakini likakataliwa na
mwamuzi Dennis Bate kutoka Uganda.
Aliongeza kuwa mchezaji Elias Pelembe aliyeifungia
Msumbiji bao la pili dakika ya 83 kwa mpira wa adhabu nje ya eneo la hatari
ndiye aliyemaliza mchezo huo. Pia ni mchezaji huyo aliyebadili matokeo ya
mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam ambapo Msumbiji ilisawazisha dakika tatu
kabla ya filimbi ya mwisho.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager, na ambayo ilicheza vizuri kipindi cha pili ilipata bao lake dakika ya 78
na Mbwana Samata kwa shuti la pembeni akiwa nje ya eneo la hatari na kumshinda
kipa Ricardo Campos.
Matokeo hayo yameipeleka Msumbiji katika kundi C
lenye timu za Cape Verde, Niger na Zambia. Mechi za hatua ya makundi kutafuta
tiketi ya kucheza fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco
zitaanza kuchezwa mwezi ujao.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es
Salaam wiki mbili zilizopita timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. Timu
itakayosonga mbele itaingia kwenye kundi lenye timu za Cape Verde, Niger na
Zambia.
Taifa Stars inarejea Dar es Salaam leo (Agosti 4
mwaka huu) saa 8 mchana kwa ndege ya Air Tanzania.
Kikosi cha Stars kilipangwa hivi; Deogratias
Munishi, Said Moradi, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Erasto
Nyoni, Mwinyi Kazimoto, Mcha Khamis/Amri Kiemba, John Bocco/Simon Msuva, Mbwana
Samata na Thomas Ulimwengu/Mrisho Ngasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WASIWASI UMEIGHARIMU TAIFA STARS- NOOIJ”
Post a Comment