Sunday, August 3, 2014
WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA AMEUAMBIA UONGOZI WA JIJI LA MBEYA UONGEZE MAPATO YA NDANI.
Do you like this story?
JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI
MKUU
WAZIRI MKUU
Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa Jiji la Mbeya uongeze mapato yake ya ndani
kwa kuweka mifumo ya kisasa ya ukusanyaji mapato.
Ametoa agizo hilo
jana (Jumamosi, Agosti 2, 2014) wakati akizindua stendi ya kisasa ya mabasi
katika eneo la Nane Nane nje kidogo ya Jiji la Mbeya.
“Nikuombe Meya
Kapunga, wewe na watu wako ongezeni mapato ya ndani ya Jiji la Mbeya. Wekeni
mifumo ya kisasa ya makusanyo inayotumia teknolojia ya habari na mawasiliano,
acheni kutumia risiti za kuandika wa mikono,” alisema.
Akizungumzia mradi
wa stendi mpya ya mabasi, Waziri Mkuu alisema ujenzi wa stendi hiyo ni miongoni
mwa kazi zilizo kwenye mradi mkubwa unaohusisha uboreshaji wa huduma na
miundombinu kwenye miji na majiji saba hapa nchini (Tanzania Strategic Cities
Programme).
Alisema mradi huo
uliibuliwa na Serikali tangu mwaka 2006 kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.
Miji na majiji mengine yanayohusika na mradi huo ni Mwanza, Arusha, Tanga,
Kigoma, Mtwara na Dodoma.
“Utekelezaji wa
miradi katika miji na majiji haya saba, umetuwezesha kupata ufadhili katika
awamu ya pili ya mradi huu ambayo itajumuisha miji 17. Tusingekubaliwa kuingia
awamu ya pili kama ninyi madiwani msingesimamia vizuri miradi hii,” alisema.
Akisoma taarifa ya
mradi huo, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Bw. Mussa Zungiza alisema ujenzi wa
stendi hiyo yenye ukubwa wa mita za mraba 30,000 utasaidia kupunguza msongamano
wa magari kwenye barabara kuu ya TANZAM ambako mabasi ya mikoani yalikuwa
yakisimama na kupakia ama kushusha abiria.
Alisema mradi huo
wa stendi ya Nane Nane uliogharimu sh. Bilioni 2.9/- ni sehemu tu ya mradi
mzima ambao thamani yake ni sh. Bilioni 31.4 ambazo zimetumika kujenga barabara
za kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 23.1, daraja moja na dampo la
kisasa la kutupia taka (sanitary land fill) katika kata ya Nsalaga.
“Hata hivyo, mradi
huo uko chini ya uangalizi wa mkandarasi hadi Desemba 4, 2014 utakapokabidhiwa
rasmi kwa Halmashauri ya Jiji, “ alisema Bw. Zungiza.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu Pinda ameutaka uongozi wa Jiji la Mbeya kuhakikisha
unatengeneza kwanza miundombinu ya maji na vyoo katika eneo jipya lililopo
jirani na stendi mpya ya Nane Nane ambalo limetengwa mahsusi kwa ajili ya
wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama ‘wamachinga’.
“Ni vema Jiji
litenge kiasi cha fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za muhimu kama maji na
vyoo badala kukimbilia kuwalundika mahali hapa. Wafanye biashara zao, na hata
mtu akitoka stendi akaja kununua bidhaa zao, kama na shida apate mahali pa
kujihifadhi,” alisema huku akishangiliwa na umati uliohudhuria uzinduzi huo.
Aliwataka
wawapangie maeneo ya mabanda yao, na ikibidi watafute mwekezaji anayeweza
kufanya kazi hiyo. “Tusifanye kosa la kuja kuwalundika tu. Ni heri kugharimika
kidogo lakini pawe pazuri. Tengenezeni eneo hili ili kituo chenu kiwe cha mfano
na wengine waje waige,” aliongeza.
Uzinduzi huo
ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi (OWM – Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu,
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Bw. George Owuor, Kaimu Balozi wa Uganda
nchini Tanzania, Bibi Nora Katabarwa, Wakuu wa Mikoa ya Rukwa, Iringa, Njombe
na Katavi ambao walikuwa jijini Mbeya kuhudhuria kongamano la Uwekezaji na
wanahudhuria maonyesho ya Nane Nane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM
JUMAPILI, AGOSTI 3, 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA AMEUAMBIA UONGOZI WA JIJI LA MBEYA UONGEZE MAPATO YA NDANI.”
Post a Comment