Sunday, August 3, 2014
WAUAJI WA KUKODI WAIBUKA TANZANIA" WANAITWA VIJANA WA KAZI"
Do you like this story?
Mitandao ya kihalifu inazidi
kujiimarisha nchini na sasa kumeibuka makundi ya wauaji wa kukodi katika mikoa
ya kaskazini mwa nchi pamoja na Kanda ya Ziwa.
Mbali na mauaji ya albino na
vikongwe ambayo yalipata kutikisa katika maeneo kadhaa ya nchi, wauaji wa
kukodi wanatumika kutekeleza uhalifu huo kwa lengo la kulipiza kisasi, uporaji
wa fedha, kujitanua kibiashara au kudhulumu mali na fedha.
Uchunguzi wa muda mrefu uliofanywa
umebaini kuwa silaha nyingi zinazotumika katika mauaji
ya kukodi yanayofanyika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, hununuliwa ama kukodishwa
kutoka Namanga upande wa Kenya.
Wauzaji wa silaha hizo ni ama raia
wa Kenya wenye asili ya Kisomali ama wahamiaji haramu wenye asili ya Kisomali
wanaoingia nchini, wakitokea Somalia kupitia Kenya.
Uchunguzi umebaini kuwa bunduki aina
ya Submachine Gun (SMG) huuzwa kati ya Sh3 milioni hadi Sh5 milioni na bastola
zikiuzwa kati ya Sh500,000 na Sh1.2 milioni.
Pamoja na kutoka nje ya nchi, wauaji
wengine wa kukodi hupatikana nchini kulingana na aina ya mtu wa kuuawa,
mazingira na ugumu wa kazi.
Kwa Tanzania, mikoa inayoongoza kwa
kuwa na wauaji wa kukodi ni Arusha na Manyara na Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa
ukiguswa kuwa jirani na mikoa hiyo.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa
jina, mtoa taarifa wetu alisema alisema: “Hata sasa ukihitaji vijana wa kazi
nitakuunganisha. Jambo muhimu hakikisha huwarushi (unawapa fedha zao),
ukiwarusha lazima na wewe watakuua.”
“Yupo rafiki yangu anayewafahamu
vyema kwa sababu amewahi kuwaunganisha na waliokuwa wakihitaji huduma yao,”
alisema mtoa habari huyo.
Malipo
ya kuua
“Malipo kwa kazi hii yanaanzia kati
ya Sh1 milioni na Sh5 milioni kutegemea na uzito wa kazi husika,” alisema mtoa
taarifa wetu anayeishi Arusha na akithibitisha kwamba anafahamiana na madalali
wa wauaji hao.
Alisema mara nyingi wauaji hao
hawataki kukutana na wateja moja kwa moja ili kuepuka kutambulika, badala yake
hukutana au kuwasiliana na mtu wa kati (wakala) ambaye pia hupokea malipo na
kuwakabidhi.
Hata hivyo, uchunguzi
ulibaini kuwa kiasi cha malipo kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini ni kikubwa
ikilinganishwa na Kanda ya Ziwa ambako hulipwa fedha kidogo.
Vyanzo hivyo vimedokeza malipo
wanayopata katika mikoa hiyo ni Kati ya Sh200,000 hadi Sh1 milioni kwa
kuzingatia eneo husika na walikotolewa na kwamba fedha hizo huwa ni ujira wa
watu wawili au zaidi.
Katibu wa Jumuiya ya Kuhifadhi Mila
na Desturi za Mtanzania Kanda ya Ziwa, Gambang’adi Kaliba anasema wanaokodiwa
ni wale wasiokuwa na vipato, walevi na wavuta bangi ambao wamekata tamaa ya
maisha, hivyo hupewa fedha kidogo kwa ajili ya mauaji hayo ya kikatili.
“Watu wanalipwa Sh200,000 mpaka
500,000 kwa kuwa hawafanyi kazi wanaziona nyingi na wamekuwa wakijulikana
katika baadhi ya maeneo kwa kuwa wakilewa hutamba na kuwa wako tayari kumwaga
damu ya mtu maadam wapewe fedha,” anasema Kaliba.
Mkoani Mara, uchunguzi ulibaini kuwa
kumekuwapo na mauaji ya aina hiyo na kwamba malipo kwa kifo cha mtu huwa ni
kati ya Sh300,000 na 500,000.
Mwanaharakati wa Haki za Binadamu
wilayani Ukerewe ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe anasema wanapowakamata
wahusika wa mauaji, baadhi hukiri kukodiwa kwa malipo ya Sh200,000 na kwamba
idadi yao huwa ni kati ya watu wawili au watatu.
Mifano
hai
Chanzo kimoja kutoka ndani ya Jeshi
la Polisi mkoani Manyara kilisema kuwa mauaji ya mmoja wa wafanyabiashara
yalifanywa kwa kutumia mtandao huo.
Aliuawa mwaka jana wilayani Hai,
Mkoa wa Kilimanjaro.
“Mirerani ndiyo umafia huo unatumika
sana unajua kule ni unyama unyama kwa hiyo mtu kukuua kwa sababu ya mawe ni
jambo la kawaida,” alidokeza polisi huyo.
Habari za kipolisi zinaeleza kuwa
wauaji wa mfanyabiashara huyo walilipwa kati ya Sh3 milioni milioni na Sh5
milioni baada ya kukodiwa mahususi kutekeleza mauaji hayo.
Bunduki aina ya SMG inayodaiwa
kutumika katika mauaji hayo ilinunuliwa kwa Sh4 milioni katika mpaka wa
Tanzania na Kenya, Namanga kutoka kwa watu wenye asili ya Somalia.
Mauaji mengine yanayofanana na hayo
yalitokea Januari 26, 2006 saa 2:30 usiku nje ya klabu maarufu ya Peters Club
iliyopo Majengo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Siku hiyo watu waliokuwa na SMG
walimmiminia risasi mfanyabiashara wa magari ya ‘dili’, Aristarik Msacky (34)
na kutochukua chochote isipokuwa simu yake ya mkononi.
Kabla ya kuuawa, mfanyabiashara huyo
alikuwa akinywa pombe na marafiki zake ndipo alipopigiwa simu ili atoke nje
kuna ‘biashara’ na alipotoka nje ya baa ili kukutana nao ndipo alipouawa.
Tukio jingine ni lile la mkazi wa
Kijiji cha Nyichoka wilayani Serengeti, Mara ambaye alituhumiwa kumuua
mwendesha pikipiki (bodaboda), Julai 5 mwaka huu ambaye kwa mujibu wa polisi,
alikiri kufanya mauaji hayo kwa kukodiwa.
Polisi walisema mtuhumiwa huyo (jina
tunalihifadhi) alikiri kwamba yeye na mwenzake ambaye aliuawa na wananchi
wenye hasira kali, walikodiwa na mkazi wa Park Nyigoti kutekeleza mauaji hayo
kwa Sh500,000 kwa madai kuwa bodaboda alikuwa na uhusiano na wake zake.
Hata hivyo, mpaka wanatekeleza mauaji
hayo kwa kumkatakata na kumtumbukiza mtoni, walikuwa wamelipwa Sh40,000 tu na
kati ya fedha hizo Sh20,000 zilikuwa za kukodi pikipiki na zilizobaki kwa ajili
ya chakula. Hadi mmoja alipouawa na yeye kukamatwa walikuwa wakimdadisi ‘bosi’
wao Sh460,000.
Msemaji
wa Polisi
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera
Senso alisema polisi wapo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia na mali zao na
hivyo ndivyo wamekuwa wakifanya kila wakati, kutimiza wajibu huo.
Senso alisema kwamba endapo
wakibaini kuwa kuna watu wanafanya uhalifu wa namna hiyo huwakatama na
kuwafikisha mahakamani, huku akitoa mwito kwa wananchi na jamii nzima kutimiza
wajibu wao wa kutoa taarifa za makundi kama hayo katika maeneo wanayoishi.
via>>Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAUAJI WA KUKODI WAIBUKA TANZANIA" WANAITWA VIJANA WA KAZI"”
Post a Comment