Thursday, October 2, 2014
02 Oct 2014 DAR ES SALAAM KUFUNGWA KAMERA ZA KISASA ZA MATUKIO.
Do you like this story?
NASRA ABDALLAH, Dar Es Salaam, Tanzania
RAIS Jakaya Kikwete, amesema kuanzia Juni mwakani
kila kinachofanyika katika jiji la Dar es Salaam kinaonekana katika mitambo
itakayokuwapo kila mahali.
Alisema kutokana na kufungwa kwa mitambo hiyo waharibifu wa miundombinu,
vibaka na wahalifu hawatoweza kufisha matendo yao.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla
ya kufungua barabara ya Tegeta – Mwenge iliyojengwa kwa kiwango cha lami huku
ikiwa na urefu wa kilometa 12.9.
Alisema inasikitisha kuona serikali ikiingia gharama kubwa katika
kutengeneza barabara halafu watu wasiokuwa na uchungu na fedha hizo za walipa
kodi wakiharibu miundombinu hiyo kwa maslahi ya matumbo yao.
“Tumeshaongea vya kutosha jamani katika hili sasa dawa ya watu wa aina
hii ipo jikoni na Juni mwakani watu wote hawa tutawakamata kirahisi tu
hawatakuwa na pa kukimbilia,”alisema.
Hata hivyo Rais Kikwete, hakuwa tayari kueleza ni mitambo ya aina gani
itakayofungwa lakini katika nchi mbalimbali kumekuwa na kamera katika mitaa
ambazo zinarekodi kila kinachofanyika.
Aliongeza kuwa ujenzi wa barabara ya Tegeta-Mwenge, itasaidia kupunguza
msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam na hii ni baada ya kukaribia
kumalizika kwa barabara ya Msata Bagamoyo.
Alisema kutokana na tatizo la foleni lililopo katika Jiji hilo, ambapo
hata mihadi ya watu kukutana siku hizi imekuwa ni taabu, Serikali imekuwa
ikijitahidi kutafuta njia mbalimbali za kutatua kero hiyo ikiwemo kuboresha
vyombo vya usafiri wa umma na utengenezaji wa barabara za mchepuko.
Hata hivyo aliwataka wananchi kujua kuwa tatizo la foleni halipo tu Dar
es Salaam bali hata kwanye nchi zilizoendelea ikiwemo Newyork Marekani na
China.
Rais Kikwete, alisema hii inachangiwa na kukua kwa maendeleo ambapo kwa
Tanzania mwaka 1980 magari yaliyokuwa yakipita barabarani ni yale ya Serikali
na kwa watu binafsi ilikuwa lazima uombe kibali kabla ya kununua gari.
“Lakini hivi sasa familia nyingi zinamiliki magari na nyingine zimeenda
mbali zaidi ambapo baba ana gari lake, mama na watoto na bado watu wataendelea
kumiliki magari siku za baadaye yote hii imechangiwa na kubadilika kwa mfumo wa
maisha na nchi kupiga hatua ya maendeleo kwa watu wake,”alisema.
Alisema ameziagiza Mamlaka husika kuboresha usafiri wa reli kwa kuongeza
njia za reli katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kuleta
mabehewa yatakayoendana mahitaji.
Alisema pia serikali ipo mbioni kuanzisha kivuko kitakachotoa huduma kwa
wakazi wa Bagamoyo na Tegeta na kujenga miji mingine nje ya mji ili huduma
zinazofuatwa mjini zipatikane huko huko walipo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Alhaj Mussa Iyombe, alisema
barabara hiyo imetengenezwa kwa msaada mkubwa wa Serikali ya Japan ambako
shilingi bilioni 99.6 zimetumika kukamilisha mradi huo.
Naye Balozi wa Japan hapa nchini, Masaki Okada, alisema Serikali yake
inaamini kuwa barabara ni kichocheo kikubwa katika ukuaji wa uchumi na
kipaumbele chake cha kwanza ni ujenzi wa barabara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ 02 Oct 2014 DAR ES SALAAM KUFUNGWA KAMERA ZA KISASA ZA MATUKIO.”
Post a Comment