Saturday, October 25, 2014
FREEMASON YAZUA KIZAAZAA KWENYE CHANJO HUKO RUFIJI PWANI
Do you like this story?
Chanjo ya surua na rubella katika baadhi ya maeneo wilayani Rufiji, Mkoa
wa Pwani imekumbwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo ya baadhi ya wananchi
kugoma kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya kwa madai kuwa dawa hizo
zinatolewa na ‘Freemason’ ili kuwafunga vizazi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Rufiji, Michael Mollel alisema jana
kuwa uvumi huo upo katika kata za Mgomba na Mlanzi.
Alisema mahudhurio ya wananchi katika vituo vya chanjo vilivyopo maeneo
hayo ni ya kusuasua, lakini kata nyingine mwitiko wake ni mkubwa.
Dk Mollel aliwataka wananchi kupuuza maneno ya mitaani ambayo hayana
ushahidi wa kisayansi, badala yake wawapeleke watoto kupata chanjo hiyo muhimu.
Alisema sambamba na chanjo za ugonjwa huo, pia kutakuwa na utoaji wa
matone ya vitamin A na dawa za kukinga magonjwa ya minyoo, matende na ngiri
maji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu alisema amekerwa
na wanaosambaza uvumi huo, huku akiwataka wananchi kupuuzia taarifa hizo za
mitaani.
“Hakuna Serikali yoyote duniani inayoweza kutoa dawa kwa ajili ya
kuathiri watu wake,”alisema.
Alisema dawa hizo ni sahihi na salama zenye lengo la kulinda afya za
watoto na hazina madhara kwa binadamu.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Donald Mbando alikaririwa akisema kuwa,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatarajia kufikia watoto zaidi ya 21 milioni
wenye umri kuanzia miezi tisa hadi miaka 15.
Lengo la kampeni shirikishi ya ugonjwa wa surua na rubella ni kuhakikisha
magonjwa yanayoepukika kwa chanjo yananatokomezwa.
Na Amini Yasini
Na Amini Yasini
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “FREEMASON YAZUA KIZAAZAA KWENYE CHANJO HUKO RUFIJI PWANI ”
Post a Comment