Monday, October 20, 2014
HOFU YA EBOLA YATANDA HUKO SENGEREMA,BINTI AZIKWA KI EBOLA EBOLA
Do you like this story?
Watu sita wakiwamo wahudumu watatu wa
afya wa hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wamewekwa chini
ya uangalizi maalum baada ya kumhudumia mgonjwa aliyefariki akiwa na dalili za
ugonjwa wa ebola.
Mtu aliyefariki alitajwa kuwa ni Salome
Richard (17), anayetoka katika kijiji cha Kahunda wilayani Sengerema mkoani
Mwanza.
Akithibitisha kuwapo kwa hali hiyo
Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema, Dk. Mary Jose,
alisema mgonjwa huyo alifikishwa katika hospitali hiyo na ndugu zake watatu
akiwa na homa kali huku akitokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili
wake.Alisema vipimo vya mgonjwa huyo vimepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili
kwa uchunguzi zaidi.
“Tulimpokea juzi saa
7 mchana kutoka katika kijiji cha Kahunda wilayani hapa akiwa na homa kali
akitokwa damu mwilini, lakini kwa tahadhari tulimweka wodi maalum peke yake
akipatiwa matibabu na ilipotimu saa 8 usiku alifariki dunia,” alisema
Alisema kutokana na
tahadhari ya ugonjwa huo, watumishi watatu wa idara ya afya na ndugu watatu wa
marehemu huyo, wamezuiliwa kwa kuwekwa katika uangalizi maalum hadi matokeo ya
vipimo vilivyochukuliwa vitakaporejeshwa toka Muhimbili.
Akizungumzia tukio
hilo, muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo, Daniel Mihayo, alisema timu maalum ya
watalaam na viongozi wa mkoa walienda hospitalini hapo juzi na kuondoka na
vipimo vya mgonjwa huyo kabla hajafariki dunia kwa kuzingatia maelekezo ya
serikali ya kuchukua tahadhari linapotokea tukio kama hilo.
“Kwa sasa jamii
inatakiwa kuepukana na uzushi uliozagaa kila kona kuhusu mgonjwa huyo kufariki
kwa ebola…tunawamba wasiwe na wasiwasi kwani hatua stahiki zinachukuliwa kwa
wagonjwa wa aina hiyo kama tahadhari,” alisema Mihayo.
Mhudumu aliyempokea
mgonjwa huyo katika hospitali hiyo, Fungameza Majula, alisema ndugu watatu
walimpeleka mgonjwa huyo kwa taksi lakini alipobaini dalili hizo aliujulisha
uongozi wa hospitali na mara moja hatua za tahadhari zilichukuliwa ikiwa ni
pamoja na kuwazuia ndugu kurudi nyumbani.
Hata hivyo, juhudi za
kumpata mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Careen Yunusu, kuzungumzia tukio hilo
hazikufanikiwa.
Akizungumzia tukio
hilo, Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza, Bw.Valentino Bangi, alisema alipokea taarifa
za mgonjwa huyo kufariki kwa homa inayofanana na ugonjwa wa ebola au maburgh.
Bw.Bangi alisema
ofisi yake imetuma timu ya wataalam wa afya katika Hospitali ya Wilaya
Sengerema na kuchukua sampuli ya vipimo vya mgonjwa na kupeleka Muhimbili kwa
uchunguzi zaidi.
Bw.Bangi alisema ili
kukabiliana na mlipuko wa magonjwa hayo, tayari taifa, uongozi wa mkoa wa
Mwanza kwa kushirikiana na ofisi yake, wameweka vituo vya kupima magonjwa
katika mipaka ya Sirari, Mutukula na uwanja wa Ndege wa Mwanza
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ HOFU YA EBOLA YATANDA HUKO SENGEREMA,BINTI AZIKWA KI EBOLA EBOLA ”
Post a Comment