Monday, October 13, 2014
KILA KATA INAPASWA IWE NA KITUO CHA AFYA - WAZIRI MKUU
Do you like this story?
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka viongozi wa mkoa wa
Tabora wajipange vizuri na kuhakikisha kuwa wanajenga vituo vya afya katika
kila kata za wilaya ya Urambo kwa sababu bado iko nyuma.
“Hatua hii itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa
kwenye hospitali ya wilaya ya Urambo kwa sababu yenyewe imekuwa ndiyo kimbilio
la kila mgonjwa kwa sasa,” amesema.
Ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na
mamia ya wakazi wa mji wa Urambo mara baada ya kuzindua jengo la Mama Ngojea
linaloitwa Mayu Lindila lililopo kwenye hospitali ya wilaya
hiyo.
“Wilaya yenu ina kata 16, ina vijiji 57 na zahanati 22
lakini ina kituo kimoja tu cha afya. Na hii maana yake ni kwamba kuna vijiji
havina zahanati kabisa. Huu ni mtihani mkubwa na ndiyo maana kila mtu akiumwa
anakimbilia kwenye hospitali ya wilaya,” alisema Waziri Mkuu.
“Kisera kila kata ni lazima iwe na kituo cha afya, kwa
hiyo viongozi wa mkoa na wilaya ni lazima mjipange kuona ni kwa namna gani
mtaitekeleza sera hii, na pia jengeni zahanati kwenye vijiji ambavyo havina
zahanati,” alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa huduma ya Mama Ngojea,
Waziri Mkuu alisema unasaidia kuokoa maisha ya mama mjamzito anayetoka kata ya
mbali ambaye anakabiliwa na tishio lakini siku zake za kujifungua zinakuwa
hazijafika.
Alisema kutokuwepo kwa majengo ya Mama Ngojea katika
maeneo mengi ni changamoto kubwa na hatari kwa akinamama wengi hasa waishio
mbali na huduma za tiba. “Hivi kama kata moja iko mbali na makao makuu ya
wilaya, na mama mjamzito mwenye tatizo hawezi kufika hospitali unadhani ataenda
wapi? Si ataenda kwa wakunga wa jadi au waganga wa kienyeji tu?”
Aliwasihi akinamama wa wilaya hiyo wajitahidi kutumia
huduma za hospitali kwa sababu kwa wakunga wa jadi na waganga wa kienyeji
hakuna wataalamu kama waliopo hospitalini.
Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bibi Fatma Mwassa afanye
utaratibu ili kila wilaya pawe na Mama Ngojea. “Hata kama hakuna hospitali ya
wilaya lakini pana kituo cha afya, ni vema pawe na jengo la Mama Ngojea ili
kuokoa maisha ya akinamama.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Mganga Mkuu wa
Wilaya hiyo, Dk. Kheri Kagya alisema jengo hilo lenye uwezo wa kulaza wagonjwa
24 kwa wakati mmoja, lilianza kujengwa Agosti 25, 2012 na lilikamilika Novemba
10, 2013 kwa gharama ya sh. milioni 198/-. Lina jiko, sehemu ya kulia, mabafu,
vyoo, eneo la kufulia na kupumzikia.
Lengo la kujenga kituo hiki ni kupunguza vifo vitokanavyo
na uzazi kutoka vifo 228 kwa kila vizazi hai 100,000 na kufikia vifo 90 kwa
kila vizazi hai 100,000 au chini ya hapo ifikapo mwaka 2015. “Mwaka 2012
tulikuwa na vifo 253 kwa kila vizazi hai 100,000 na mwaka jana tulikuwa na vifo
228 kwa kila vizazi hai 100,000. Nia yetu ni kupunguza kabisa vifo vya
akinamama kabla na wakati wa kujifungua,” alisema.
Aliwashukuru Mbunge wa jimbo la Urambo ambaye pia ni
Waziri wa Afrika Mashariki, Bw. Samuel Sitta na mkewe Mama Margareth Sitta
(ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa huo) kwa kubuni wazo hilo na
kutafuta fedha za kujenga Mama Ngojea kwenye hospitali ya wilaya hiyo.
Wakati huohuo, Bwana na Bibi Sitta wamechangia mablanketi 300 na
vyandarua 100 kwa ajili ya Mama Ngojea pamoja na hospitali ya wilaya hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “KILA KATA INAPASWA IWE NA KITUO CHA AFYA - WAZIRI MKUU ”
Post a Comment