Friday, October 31, 2014
MAAFISA WALIOBAINISHA UFISADI WA BILIONI 40 WATISHIWA KIFO
Do you like this story?
SAKATA la ubadhirifu wa bilioni 40
katika halmashauri ya jiji la Mwanza limechukua sura mpya baada ya maofisa wa
ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) walioibua sakata hilo
kudai kutishiwa maisha.
Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Rajab Mohammed
Mbarouk wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara yao mkoani hapa ambacho
hakikuendelea kufanyika kutokana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia
au mwakilishi wake kutofika katika majumuisho hayo.
“Tumepokea taarifa ya kutishiwa amani
kwa baadhi ya wakaguzi, tunasema ofisi ya CAG ipo kisheria na kikatiba na
wanafanya kazi kwa kufuata sheria na Katiba,” alisema Mbarouk na kuongeza kuwa,
kama wabunge watahakikisha wanatunga sheria na kuzisimamia na kwamba wakaguzi
waendelee na kazi yao bila ya hofu.
Mbarouk alimpongeza Mkaguzi Mkazi
pamoja na timu yake kwa kuwa na uzalendo wa kitanzania wa kutaka kuokoa uchumi
wa Mwanza ambao kwa asilimia 90 unahujumiwa.
Alisema uchumi wa Mwanza unatokana na
mapato na miradi ya maendeleo ambapo maeneo hayo yakifanyiwa kazi isiyoridhisha
CAG anawajibu wa kutoa taarifa.
Alisema kama Mkaguzi Mkazi ameweza
kuwasilisha taarifa yake kwa Bunge pamoja na kwa Rais. Awali, Mjumbe wa kamati
hiyo, Kange Lugora alisema kamati hiyo iliishauri wizara husika kushirikiana
nao pamoja tangu mwanzo wa ziara yao katika majumuisho ya kamati hiyo ili
kubaini yanayotendeka katika miradi ya maendeleo.
“Kitendo cha wizara kutoshiriki katika
majumuisho ya kamati hii ni kuendelea kuhalalisha ubadhirifu unaoendelea kwenye
halmashauri, tunaonyeshwa miradi hewa na serikali ngazi ya wizara ilipaswa wajionee
wenyewe,” alisema.
Aliongeza kuwa, ili waweze kuwatendea
haki Watanzania na wana Mwanza, kamati iliagiza kuwa hawawezi kuendelea na
mahesabu ya halmashauri ya jiji la Mwanza hadi wizara itakapomrudisha
Mkurugenzi wa zamani wa jiji hilo, Wilson Kabwe ambaye kwa sasa amehamishiwa
Dar es Salaam.
Alisema kwamba wizara haijafanya
jitihada za kumrejesha mkurugenzi huyo na kudai kuwa mazingira hayo yanawafanya
washindwe kuwatendea haki Watanzania.
Alisema ili kamati ilinde heshima yake
na kwa mazingira hayo hawataweza kufanya majumuisho kwani kwa kufanya hivyo ni
kuwasaliti Watanzania.
Grace Chilongola, Mwanza
A
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAAFISA WALIOBAINISHA UFISADI WA BILIONI 40 WATISHIWA KIFO ”
Post a Comment