Saturday, October 4, 2014
SAMUEL SITTA, NISINGESHIRIKI KARAMU YA WENYE DHAMBI
Do you like this story?
Kwako
mheshimiwa Samuel Sitta.
Ni matumaini yangu kwamba sasa unajipongeza kwa kufanikisha kazi
uliyopewa ya kuliongoza Bunge Maalum la Katiba ya kuhakikisha akidi inatimia
ili kupitisha rasimu ya katiba inayopendekezwa.
Najua una furaha sana kwa hilo, upo kwenye karamu ya kufurahia ushindi
kiasi kwamba itakuwa vigumu sana kwa lofa kama mimi kukutana na wewe hasa
katika kipindi hiki ambacho unaamini kasi na viwango vyako vimedhihirika. Hata
hivyo, hilo halinizuii kufikisha ujumbe wangu kwako.
Mimi si Mbunge wa Urambo Mashariki kama wewe, sikuzaliwa Desemba 18, 1942
wala sijamuoa mwanamke mwanasiasa, Magreth Sitta aliyewahi kushika nyadhifa
mbalimbali serikali kama wewe. Mimi ni mwananchi wa kawaida tu, lofa, hohehahe
nisiye na mbele wala nyuma.
Sijawahi kuwa spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wala
sijawahi kujipatia umaarufu mkubwa na kupendwa na wengi kutokana na kuruhusu
mijadala ya ufisadi bungeni kama ulivyo wewe. Sijawahi kuibua kashfa kubwa kama
ya Richmond na kusababisha baadhi ya vigogo wang’atuke kwenye nyadhifa zao.
Sina nia wala sitegemei kuja kugombea urais wa nchi hii kama wewe, mimi
ni mwananchi wa kawaida kabisa. Sijawahi kujisifu kwamba mimi ni mtu wa viwango
na kasi, mimi ni mlala hoi tu.
Sijawahi kuitumia nchi hii katika nyadhifa mbalimbali kuanzia nilipokuwa
shule, kwa zaidi ya miaka 40 nikigusa karibu awamu zote za uongozi kama wewe,
mimi si Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wala sijawahi kuota ndoto
kwamba nitakuja kuwa Spika wa Bunge Maalum la Katiba! Narudia tena, mimi ni
mwananchi wa kawaida kabisa, hohehahe nisiye na ndoto za kuja kuwa mwanasiasa.
Hata hivyo, ningekuwa mimi ndiyo nipo kwenye nafasi yako, hakika nakuapia
nisingeshiriki kwenye karamu ya wenye dhambi kama wewe. Nisingeshiriki hata
kidogo kuchakachua maoni ya mwenyekiti wa tume ya kukusanya maoni kuhusu katiba
mpya, Jaji Joseph Warioba kama wewe.
Nisingerudia kukusanya upya maoni kwa wananchi wakati nikijua fika kuwa
hiyo siyo kazi yangu. Nisingebadilika ghafla kama wewe, kutoka kuwa shujaa wa
kutegemewa kama ulivyokuwa kipindi ulipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano na kuwa adui wa demokrasia kama ulivyo sasa.
Nakuhakikishia nisingeshiriki kabisa karamu ya wenye dhambi, kwa
kulazimisha wajumbe wa bunge maalum la katiba, hata kwa vitisho waipigie kura
ya ndiyo rasimu ya katiba inayopendekezwa huku nikijua waziwazi kwamba
nimeshiriki kunyofoa vipengele vyote muhimu ambavyo wananchi walivipendekeza
ili kupata katiba bora.
Nisingefikia hatua ya kuwatusi viongozi wa dini ambao walikuwa
wakinionesha waziwazi kwamba nilichokuwa nakifanya kwenye bunge maalum la
katiba hayakuwa matakwa ya Mungu bali ya watu wachache wenye dhambi.
Kwa kuwa najua kwamba katiba ndiyo ‘injini’ ya maendeleo ya taifa lolote,
ningekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba maoni ya wananchi ndiyo
yanayoingia kwenye katiba bila kuchakachuliwa. Ningethibitisha kwa vitendo
kwamba mimi ni mtu wa kasi na viwango!
Nisingekubali kuongozwa na tamaa ya kuja kuwa rais wa nchi hii kiasi cha
kulipua mchakato mzima wa kupata katiba kwa maslahi yangu na chama changu kwa
sababu ningejua kwamba umri umeshanitupa mkono (Una miaka 71 sasa) lakini wapo
wanangu, wajukuu na ndugu zangu wengi na watu wanaoniamini ambao wanaisubiri
kwa hamu katiba mpya itakayowakomboa, baada ya ile ya awali kushindwa
kuwatatulia kero zao kwa zaidi ya miaka hamsini sasa.
Narudia tena, nisingeongozwa na tamaa ya madaraka, upendeleo kwa chama
changu wala maslhai ya mtu au watu fulani, la hasha! Ningesimamia haki katika
ukamilifu wake na rasimu ambayo ingepatikana, ingekuwa ni mawazo ya wananchi
wote na siyo uhuni kama uliofanyika sasa kupata rasimu ya katiba
inayopendekezwa.
Ningeongozwa na hofu ya Mungu na nisingewaangusha wananchi ambao kwa
kipindi kirefu waliniona mpiganaji ninayesimamia maslahi yao na taifa kwa jumla
na kamwe nisingeshiriki karamu ya wenye dhambi kama ilivyotokea kwenye Bunge
Maalum la Katiba.
Kwa bahati mbaya mimi nitabaki kuwa mimi na sitaweza kuwa wewe lakini
kama ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, kwa jinsi hali ilivyo sasa, narudia
tena kusema bila kumung’unya maneno kwamba nisingeshiriki kwenye karamu ya
wenye dhambi kama wewe, ningesimamia ukweli, haki na demokrasia bila
kumpendelea wala kumkandamiza mtu yeyote.
Wasalaam!CHANZO GLOBAL PUBLISHER TANZANIA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SAMUEL SITTA, NISINGESHIRIKI KARAMU YA WENYE DHAMBI ”
Post a Comment