Friday, October 3, 2014

PINDA ATAMANI KURA KABLA YA UCHAGUZI MKUU .




WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema ana shauku kuona Katiba Inayopendekezwa, inapigiwa kura na Watanzania na kuwa Katiba kabla hata ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani, kwa kuwa ikiachiwa kuna watu wanaweza kuleta vurugu.

Alisema kazi iliyobakia ni kupeleka Katiba hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

“Mimi naamini hata ikibidi tupige kura zote mbili kwa wakati mmoja, ya kwanza ya kumchagua Rais na nyingine ya kupitisha Katiba.

“Mama zangu nyie nguvu yenu ni kubwa na tunaihitaji sana…mkijipanga vizuri na kutaka hili lifanyike litafanikiwa hata bila nguvu yetu wanaume,” alisema Pinda.

Kauli hiyo ya Pinda, inaweza kutafsiriwa vibaya kwamba anataka kukiuka makubaliano ya vyama vya siasa na Rais Kikwete, ya kuahirisha mchakato wa Katiba ili Katiba iliyopo irekebishwe kupisha kwanza Uchaguzi Mkuu.

Vyama hivyo vinataka mchakato wa Katiba mpya ikiwezekana, uanze upya baada ya Uchaguzi Mkuu ujao kumalizika na kupata Rais mpya wa Awamu ya Tano na wabunge.

Wakati huo huo, Pinda amesema ili Katiba Inayopendekezwa iwafikishe Watanzania ilikokusudia, wananchi wanatakiwa kukataa amani ya nchi kuchezewa.

Akizungumza baada ya kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa jana bungeni, Pinda alisema wapo watu ambao kila wakikaa wanawaza namna ya kuvuruga amani.

“Katika suala la amani, nitaendelea kupigania nchi hii na kuilinda ili ndoto ya maendeleo kwa Watanzania itimie,” alisema Pinda na kuelezea alivyofurahishwa na Sura ya Pili ya Katiba hiyo.

Sura hiyo ya Pili, imeweka malengo ya kitaifa, ambapo imeyagawa katika malengo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na katika uchumi ikisisitiza Serikali kujenga ustawi sawia wa Watanzania.

“Nimejifunza mengi na kubwa nimeona watu tumekuwa na dhamira moja kwa umoja wetu na lengo moja la kujenga Taifa moja,” alisema Pinda.

Alisema kabla ya kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa, kila mjumbe alikuwa na hofu iwapo theluthi mbili ya kura itapatikana na hasa upande wa Zanzibar, lakini imepatikana.

“Sasa wale waliotutakia mabaya sijui watasema nini,” alisema Pinda akishukuru wajumbe kutoka Zanzibar kwa kumpa nguvu huku akimtaka Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, kupeleka salamu za shukrani kwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Aliwataka Watanzania wasome Katiba Inayopendekezwa, kwa kuwa ina mambo mazuri na kuongeza kuwa imekamilika wakati mzuri ikiwa na malengo ya kiuchumi, wakati mwakani Serikali ikiandaa mpango wa miaka mitano. Kwa mujibu wa Pinda, muda wote waliokaa Dodoma kujadili Katiba hiyo, amejifunza kuwa Watanzania wanaweza kushindana kwa hoja na kupingana bila kuachana na hivyo umoja wa nchi utaendelea kuimarika.

“Kwa nguvu hii niliyoiona na umoja wetu kama tukitoka nao na kwenda kwa wananchi, hakuna litakaloshindikana,” alisema.

Alisema amefuatilia namna kila sehemu kulivyokuwa na mjadala wa nguvu, lakini mwishowe kukawa na maridhiano, jambo lililodhihirisha kuwa sauti ya wengi ni ya Mungu.

“Mimi nimekaa pale Ikulu mara zote mzee Kingunge (Ngombale Mwiru), amekuwa akiapa bila kushika Bibilia wala Kurani, lakini leo kwa mara ya kwanza amesema tumshukuru Mungu,” alisema Pinda.

Alisema kwa namna walivyokuwa wakijadili na kupingana na jana wameikubali Katiba Inayopendekezwa kwa pamoja, haamini kama kuna mtu anaweza kuipinga

0 Responses to “ PINDA ATAMANI KURA KABLA YA UCHAGUZI MKUU .”

Post a Comment

More to Read