Thursday, October 16, 2014
WAZIRI KOMBANI ANUSURU AJIRA ZA MKUU WA WILAYA NA MKURUGENZI WA ULANGA
Do you like this story?
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani ametoa msaada muhimu wa Sh milioni 40 na bati 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule 12 za sekondari zilizopo katika jimbo la Ulanga Mashariki wilayani humo, mkoani Morogoro.
Mbali na msaada huo
pia amesaidia vifaa mbalimbali ikiwamo sare, viatu na vyakula vyenye thamani ya
Sh milioni 7.2 kwa askari wa jeshi la Mgambo wa wilaya ambao wanatumika
kufyatua matofali kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara.
Kombani ambaye ni
Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki alikabidhi misaada hiyo kwenye ziara yake
aliyoianza jimboni humo jana, ambapo alisema ameamua kusaidia ujenzi huo wa
maabara ili jimbo la Ulanga Mashariki liweze kutoa wanafunzi wenye utaalamu wa
masomo ya sayansi katika siku za usoni.
Kutolewa kwa msaada
huo kwa wilaya hiyo kunaweza kufanikisha utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya
Kikwete alilolitoa kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa
mikoa wawe wamekamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kila shule ya
sekondari ya kata ifikapo Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa agizo
la Rais, kiongozi yeyote katika ngazi za wilaya na mkoa kote nchini
atakayeshindwa kutimiza wajibu kwa kutekeleza agizo hilo, atachukua maamuzi
magumu dhidi yake.
Hata hivyo alisema,
ili kufikia muda uliopangwa wa kukamilika kwa maabara hizo wameamua kuwatumia
askari wa mgambo kwa ajili ya kutengeneza matofali na ujenzi huo, ikiwa ni
sehemu ya mchango wao katika kuleta maendeleo.
“Mimi nilishaanza kwa
baadhi ya shule za jimboni mwangu kujenga vyumba vya maabara kabla
ya agizo la rais, kwa hiyo huu ni mwendelezo na nia yangu ni kuhakikisha
wana Ulanga wanasoma masomo ya sayansi kwa vitendo kwani dunia ya sasa ni
sayansi na teknolojia,” alibainisha Waziri Kombani.
Hata hivyo alitumia
fursa hiyo kwa kusema katika mafunzo yajayo ya mgambo atajitahidi
kuwapeleka wakufunzi wa masuala ya ujasilimali ili wakati wanapata
mafunzo pia wafundishwe namna ya kuendesha ujasilimali na sio ulinzi pekee ili
waweze kujikwamua kwa kuongeza kipato.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Isabela
Chilumba, alisema ujenzi wa vyumba vya maabara unaendelea na wananchi
wameshahamasishwa kupitia mikutano mbalimbali kwa ajili ya kuchangia chochote
ili kukamilisha ujenzi huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI KOMBANI ANUSURU AJIRA ZA MKUU WA WILAYA NA MKURUGENZI WA ULANGA ”
Post a Comment