Wednesday, November 5, 2014

WALIMU WATUMIA MIHOGO KAMA CHAKI KUANDIKIA PINDI WAFUNDISHAPO




Walimu wawili wanaojitolea katika Shule ya Msingi Msali,
Kata ya Nyakahura, wilayani Biharamulo, mkoani Kagera wanatumia vipande vya
mihogo mikavu na mkaa kuandikia ubaoni baada ya kukosa chaki.

Wakizungumza shuleni hapo juzi, walimu hao walisema hawana
chaki za kuandikia na kwamba wanatumia vitabu viwili vya hesabu na kiswahili
kufundishia wanafunzi 200.







Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Evelina Jeremiah alisema shule
hiyo ilianzishwa mwaka mmoja uliopita kutokana na uwapo wa watoto wengi ambao
hawajaenda shule lakini haijasajiliwa.

Alisema baada ya kuwa na idadi kubwa ya watoto, wazazi
walianzisha banda la kuwafundisha kusoma, kuandika na kuhesabu hali
iliyosababisha kuajiri vijana waliomaliza kidato cha nne kuwafundisha.

Jeremiah alisema licha ya kukosa chaki na vitabu, kuna
upungufu wa madawati na madaftari kwani wanafunzi hao hawapati mahitaji muhimu
ya shule ukilinganisha na wenzao wa shule nyingine za Mzani na Nyakahura.

“Tunafundisha kwa taabu maana hata mshahara tunalipwa na
wazazi Sh30,000 kwa mwezi, lakini kupatikana kwake ni kuvutana na kutufanya
tuishi maisha ya ombaomba,” alisema.

Naye Mwalimu Robert Mussa alisema matatizo mengine ni kuvuja
kwa jengo linalotumika kama darasa wakati wa mvua na kuathiri ufundishaji.

Diwani wa Kata ya Nyakahura ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, Apolinary Mugarula alikiri kuwapo kwa
shule hiyo na kwamba, ilianzishwa kinyemela na wafugaji wa eneo hilo bila
usajili.

Mugarula alisema tayari uongozi wa kata umetoa maagizo kwa
walimu wa shule hiyo kufuata chaki Shule ya Msingi Mzani na vitabu vya
kufundishia, wakati utaratibu wa kuisajili ukiendelea.

Alisema matatizo ya shule hiyo ni mengi hasa madarasa, vyoo,
madawati na nyumba ya walimu.

Diwani huyo wa Kata ya Nyakahura aliongeza kwamba, kubwa
zaidi ni kuwaweka walimu waliopitia mafunzo chuoni badala ya vijana wasiotambua
maadili ya utumishi kitaaluma.

Na Shaaban Ndyamukama-Biha
r

0 Responses to “WALIMU WATUMIA MIHOGO KAMA CHAKI KUANDIKIA PINDI WAFUNDISHAPO”

Post a Comment

More to Read