Thursday, January 29, 2015
JANUARY MAKAMBA NA NDOTO YA VITUO VYA MICHEZO VYA KANDA.
Do you like this story?
Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Bumbuli na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Habari na Masoko ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambaye hivi karibuni pia ametangaza nia ya
kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa January
Makamba(Pichani juu) hivi karibuni ameainisha adhma yake ya kuinua
kiwango cha michezo nchini.
Azma hizo zimo katika katika mazungumzo yake na Padre Privatus
Karugendo ambayo yamechapishwa katika kitabu ambacho gazeti hili imekipata
nakala yake ambapo ameainisha azma ya kujenga vitua vya michezo vya kanda
vyenye hadhi ya kiolimpiki.
Kwenye kitabu hicho, Makamba amejibu swali kwamba kitu gani kifanyike ili
Watanzania waweze kujivunia wanamichezo wao. Makamba alisema, “Inafedhehesha
sana kuona kwamba asilimia 79 ya Watanzania walikuwa hawajazaliwa mara ya
mwisho tumeshiriki katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika.
Mwaka huo huo wa 1980 ndio mara ya kwanza na ya mwisho tuliweza kushinda
medali za Olimpiki. Rafiki yangu Mzee Suleiman Nyambui na Mzee wetu Filbert
Bayi ndio walitutoa kimasomaso kipindi kile. Ni muhimu kurekebisha hili.”
Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania imekuwa kama kichwa cha
mwendawazimu katika medani ya kimataifa huku tasnia ya michezo ikiendelea
kugubikwa na migogoro isiyokwisha. Kutokana na migogoro hii, Tanzania
inaendelea kupoteza matumaini ya kung’aa katika medani za kimataifa.
Katika mazungumzo hayo na Padre Karugendo, Makamba alinukuliwa
akisema, “Lazima tutambue kwamba maendeleo ya michezo yanatokana na vitu muhimu
vitatu. Kwanza, ni lazima kuwepo na vipaji, bahati nzuri nchi yetu ina vipaji
vya kutosha katika aina zote za michezo. Pili, ni miundombinu na mfumo wa
kubaini na kuviendeleza vipaji hivyo, hii bado ni changamoto . Tatu, ni
utawala, uongozi, na uendeshaji wa tasnia ya michezo, hii pia ni changamoto.
Hivi vitu vitatu ni lazima viwepo ili tuweze kupata mafanikio kwenye medani ya
michezo.”
Kama mgombea wa kwanza kutangaza nia yake ya kugombea nafasi ya Urais
katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, Makamba anaungwa mkono na vijana
wengi kutokana na kuendesha siasa zake kisasa, kibunifu na kuepuka malumbano ya
jukwaani.
Katika mazungumzo hayo Makamba alielezea fikra zake alizonazo hasa hasa
kwenye kuendeleza vipaji vya Watanzania ambapo alisema, “Ni lazima tuanzishe
vituo vikubwa vya michezo au ‘sports academies’ kwenye kila kanda ya nchi yetu
vyenye hadhi ya Kiolimpiki.”
Makamba aliongeza kwamba, “Kutakuwa na vituo sita vya aina hii
katika nchi yetu ambavyo vitazungukwa na shule za msingi na sekondari za
‘boarding’. Vituo hivi vitakuwa na lengo la kukusanya wanafunzi wote kwenye
kanda husika ambao wameonekana kuonyesha vipaji ambavyo vinapaswa kuendelezwa.
Ukweli ni kwamba bila kuendeleza vipaji katika mazingira mazuri, basi tusahau
kabisa kufanya vizuri kwenye michezo. Hili linaweza kufanywa kwa ushirikiano wa
serikali na sekta binafsi”.
Mheshimiwa January Makamba anakuwa mgombea wa kwanza wa Urais kuweka
bayana mipango yake ya Tanzania Mpya katika maandishi. Anaendelea kufunguka
kwamba katika tasnia ya michezo ni muhimu sana kuwekeza katika watoto. Zaidi ya
hapo, kila timu ya ligi kuu ni lazima iwe na akademi na TFF iendeshe ligi kuu
ya timu za watoto.
“Tufikie wakati ambapo timu za taifa za miaka 10 ijayo ziwe zinaandaliwa
kuanzia sasa, na serikali itenge bajeti kila mwaka kwa timu hizo ili
kuziwezesha kukaa kambini, kufanya mechi za majaribio na kuziwezesha kushiriki
kikamilifu katika mashindano ya kimataifa. Mimi sio muumini wa hizi kamati za
zimamoto kusaidia timu ishinde ghafla ghafla wakati siku zote watu hawafanyi
maandalizi ya muda mrefu” alimalizia Makamba.
Makamba pia aligusia kuhusu suala la ukata na ufinyu wa bajeti unaokabili
tasnia za michezo. Siku zote tunaona timu za taifa za olimpiki au jumuiya ya
madola kukosa fedha za kukaa kambini ambapo huchangia katika matokeo hafifu.
“Huko nyuma, taasisi na mashirika ya umma yalikuwa na timu za michezo
zilizokuwa zinafanya vizuri na kutoa michango kwenye maendeleo ya michezo. Kwa
mfano, Pamba ya Mwanza, Sigara, Reli ya Morogoro, ushiriki huu ulichangamsha
sana michezo na ni lazima turudishe utamaduni huu,” alimalizia Makamba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “JANUARY MAKAMBA NA NDOTO YA VITUO VYA MICHEZO VYA KANDA.”
Post a Comment