Tuesday, February 3, 2015
WABUNGE WAOMBA WANAUME WAFUNGWE KIZAZI.
Do you like this story?
Wabunge wametaka kuwepo na udhibiti wa
ongezeko la watu nchini kwa kutaka wanaume wadhitibiwe katika uzazi, kama
ilivyo kwa wanawake huku wengine wakitaka serikali kuboresha rasilimali bila
kudhibiti uzazi.
Miongoni mwa waliotaka wanaume wafungwe
kizazi kama inavyofanyika kwa wanawake ni Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki,
Celina Kombani ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma.
Wakichangia mada katika semina ya Sensa
ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 kwa wabunge, iliyoandaliwa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) walisema ni vyema kuwa makini katika kudhibiti uzazi, kwani
inaweza kusababisha athari za baadaye kuwa na wazee wengi kuliko vijana.
Mbunge wa Dole, Sylvester Mabumba (CCM)
alisema hakuna haja ya kuogopa kuongezeka kwa watu, bali rasilimali zitumike
vizuri kwa kutunga sheria maalumu ya kubana mafisadi kwa kuwafilisi.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, God ole
Medeye alishauri kuwa si vyema kudhibiti uzazi, kwani kuna nchi walifanya hivyo
sasa wamebaki na wazee tu hivyo ni vyema kuangalia hali ya uchumi na uzazi.
Kombani alisema kumekuwa na suala la
uzazi wa mpango kwa wanawake tu, hivyo katika kudhibiti idadi ya watu ni vyema
wanaume nao wakadhibitiwa kwa kufungwa uzazi.
Alisema ikiwa familia inataka kudhibiti
kuzaa ni vizuri mwanamke akifunga kizazi na mwanamume naye afunge kuzaa.
Huku akiungwa mkono na Mbunge wa
Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) aliyesema ni vyema kudhibiti wanaume katika
uzazi kwa kuwa na idadi sawa kati ya wanawake na wanaume.
Mbunge wa Rungwe Magharibi,
Profesa David Mwakyusa alisema kuwadhibiti wanaume ni jambo la muhimu, kwani
iwapo mwanamume atakuwa amechepuka mara 100 atazaa watoto 100, lakini mwanamke
akichepuka mara 100 atazaa mtoto mmoja.
Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF)
alisema kudhibiti kuzaa ni kupinga vitabu vya dini vilivyosema kuzaana sana
kwani kila mtoto anakuja kwa riziki yake huku akibainisha wazi kuwa ana watoto
12 na anatarajia kufikisha 20 kwani kuna faida wapo wenye uwezo tofauti.
Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM)
ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alisema ni vyema kuangalia mifano ya Japan
na Norway na pengine walipodhibiti uzazi na sasa wanaona athari yake, hivyo ni
vyema kuwaachia wataalamu kupata uwiano wa kuzaa idadi ya watoto
wanaotakiwa kuzaliwa.
Akihitimisha majadiliano hayo, Waziri
wa Fedha, Saada Mkuya alisema tatizo la ongezeko la watu nchini ni kubwa na
lazima kujipanga kudhibiti uzazi, kwani itapunguza masuala mbalimbali.
Alisema ukizaa watoto wachache ni
lazima mke na watoto kuwa na afya njema huku huduma za elimu na afya kuwa
njema, kwani hata China walidhibiti uzazi na sasa wanalegeza masharti baada ya
kuona matunda yake, kwani ardhi haiongezeki bali watu wanaongezeka.
Akifungua semina hiyo, Waziri Mkuu
Mizengo Pinda alitaka wabunge kuhakikisha ongezeko la watu nchini,
linaendana na ukuaji wa uchumi wa asilimia 7 kwa muongo mmoja.
Alitaka kuhimiza matumizi bora ya
uzazi wa mpango katika kaya, Sera ya Idadi ya Watu na Makazi mwaka 2006 haina
budi katika suala la ongezeko la watu.
Alisema
hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Uchukuzi, Samuel
Sitta na kusema idadi ya watu nchini imeongezeka kutoka watu
milioni 34.4 mwaka 2002 hadi milioni 44.9 mwaka 2012. Alisema watu wengi
Tanzania ni watoto ambao ni asilimia 43 ya Watanzania wote wenye umri chini ya
miaka mitano.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WABUNGE WAOMBA WANAUME WAFUNGWE KIZAZI.”
Post a Comment