Thursday, March 26, 2015

ASKARI MAGEREZA WAKAMATWA NA NOTI BANDIA NA SARE ZA JESHI LA POLISI






Jeshi la polisi mkoani Simiyu linawashikilia askari wawili wa jeshi la magereza na polisi kwa kukutwa na noti bandia ikiwa ni pamoja na sare za jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ).
Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa jeshi la polisi Mkoani Simiyu Charles Mkumbo alisema kuwa askari hao walikamatwa juzi majira ya saa 9 mchana katika mtaa wa Old Maswa kata ya Nyakabindi Wilayani Bariadi.

Akizungumzia tukio hilo alisema askari hao walifika kwenye kibanda cha M-pesa kinachomilikiwa na Mwalimu wa Shule ya sekondari Old Maswa Kassian Luhende (29), wakiwa na pikipiki yenye namba za usajili T-403 CXW aina ya Sunlg kwa lengo la kuweka fedha hizo kweye simu.

Katika kituo cha kuwekea pesa, baada ya Mwalimu huyo kupokea fedha kiasi cha noti 10 zenye thamani ya Shilingi 10,000 alizitilia shaka ambapo alipoendelea kuzikagua zaidi alizigundua kuwa siyo fedha halali.

Mkumbo alieleza kuwa Mwalimu huyo baada ya kugundua fedha hizo kuwa ni feki, alichukua jukumu la kuwajulisha majirani zake ili kuomba Msaada wa kuweza kuwakamata askari hao baada ya kugundua siyo watu wema.

Aidha alieleza kuwa baada ya mwalimu kutoa taarifa kwa majirani, wananchi walikusanyika na kuanza kuwahoji askari hao, ndipo askari mmoja alipotoa kitambulisho kuwa yeye ni askari na mwingine kujitambulisha kuwa ni dereva bodaboda.

Mkumbo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni askari mwenye namba H 2420 PC Seleman Juma (25) ambaye ni askari wa kikosi cha kutuliza gasia FFU Mkoani Simiyu, na askari namba B.6499 WDR Edmund Masaga (28) ambaye ni askari Magereza wilayani Bariadi.

Kamanda Mkubo alieleza kuwa baada ya askari hao kukamatwa mmoja wao PC Selemani Juma alipopekuliwa katika mfuko wa suruali yake alikutwa na noti zingine za Bandia za elfu kumi kumi na jumla yake kama zingelikuwa halali zingelikuwa na thamani ya Shilingi 1,920,000.

Askari huyo alipokwenda kupekuliwa nyumbani kwake alikutwa na sare za JWTZ ambazo ni Pensi 4, T-shirt 2, Kombati 1 pamoja na Kitambaa.

Mkuu huyo wa polisi alieleza kuwa uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa usambazaji wa noti bandia ndani ya mkoa huo, huku akieleza kuwa mara baada ya uchunguzi kukamilika askari hao watachuliwa hatua za kinidhamu pamoja na kisheria.

0 Responses to “ASKARI MAGEREZA WAKAMATWA NA NOTI BANDIA NA SARE ZA JESHI LA POLISI”

Post a Comment

More to Read