Wednesday, April 1, 2015
MAMA ANAWA MIKONO UGONJWA WA BANZA.
Do you like this story?
MAMA
mzazi wa mwanamuziki nyota wa muziki wa dansi aliye mgonjwa, Ramadhan Masanja
‘Banza Stone’ aitwaye Khadija, amenawa mikono kuhusiana na ugonjwa wa mwanaye,
akisema akiwa mzima, alifanya kila aliloweza kumshawishi aache pombe, lakini
hakufanikiwa, kwani anaamini maradhi yake pamoja na mambo mengine,
yamesababishwa pia na kilevi.
Akizungumza nyumbani kwake Sinza-Kijiweni,
jijini Dar es Salaam, Bi. Khadija alisema hali ya mwanaye hivi sasa bado ni
tete, kwani hasikii kiasi cha kufanya mawasiliano kwa tabu na kwamba hata
kuinuka kitandani ni shida.
“Mwanangu nilikuwa namwambia kila siku,
aachane na ulevi lakini hakutaka kunisikia, ungekuta hayupo kwenye hali hii,
huu ni ubishi wake, mimi namwachia Mungu ndiyo aamue maana sina uwezo wa
kumfanya anyanyuke kitandani, kikubwa tunachofanya ni kumhudumia tu,” alisema
kwa huzuni.
Katika hali nyingine, Banza ni kama
aliyechanganyikiwa kwani anachoulizwa sicho anachojibu na hata akiimba wimbo,
anamtaja mwimbaji ambaye siyo. Aidha, maneno mengi anayozungumza hivi sasa
yanakuwa hayaeleweki.
Wakati mama mzazi akitoa matamshi hayo,
wanafamilia wengine walipoulizwa kuhusu mwitikio wa wasanii wenzake kwenda
kumjulia hali, wakiwemo aliofanya nao kazi, walisema tangu aanze kuumwa kiasi
cha mwezi mmoja uliopita, hakuna msanii aliyewahi kwenda kumjulia hali.
“Unajua kumjulia mtu hali ni moyo wa mtu,
hivyo hatuna la kusema zaidi ya kuendelea kumhudumia ndugu yetu,” alisema kaka
yake Banza aliyejitambulisha kwa jina la Hamis.
Hii siyo mara ya kwanza kwa msanii huyo
kupatwa na maradhi yaliyomlazimisha kulala nyumbani kwa muda mrefu na wadau
mbalimbali kwa nyakati tofauti wamekuwa wakihusisha hali hiyo na unywaji pombe
wa kupitiliza.
Nyota huyo pia amewahi kuzitumikia kwa
mafanikio makubwa Bendi za African Stars ‘Twanga Pepeta’, Tanzania One Theatre
(TOT), Extra Bongo na Bambino Sound.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAMA ANAWA MIKONO UGONJWA WA BANZA.”
Post a Comment