Saturday, April 25, 2015
MOROGORO: 20 MBARONI KWA KUMPIGA ASKARI POLISI.
Do you like this story?
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Leonard Paul. |
WATU 20 wamekamatwa na Polisi baada ya
kumjeruhi askari aliyekuwa doria. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro,
Leonard Paulo alisema watu hao 20 wanatuhumiwa kumpiga na kitu butu kichwani
Askari Polisi mwenye namba F 3328 Cpl Ramadhani akiwa kwenye doria na mwenzake.
Pia kamanda huyo alisema Polisi inamshikilia
mkazi wa Mawenzi mjini hapa, Dikanyo Ramadhani (29) kwa kupatikana na kete 87
za dawa za kulevya aina ya heroin ambazo thamani yake haikuweza kujulikana mara
moja.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa Aprili 23, mwaka
huu majira ya saa nne usiku katika maeneo ya Soko kuu la Manispaa ya Morogoro.
Alisema Polisi waliokuwa doria maeneo hayo
walimtilia shaka mtu huyo na baada ya kumpekua kwenye mifuko yake ya suruali
walimkuta akiwa na kete hizo 87.
Akizungumzia tukio la kupigwa askari, Kamanda
huyo alisema watu 20 wakazi wa Mindu na Sangasanga, Manispaa ya Morogoro
walimshambulia kwa kumpiga na kitu butu kichwani askari wa jeshi hilo mwenye
namba F 3328 Koplo Ramadhani.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, askari huyo baada
ya kupigwa na watu hao alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa
Morogoro ambako amelazwa na anaendelea vizuri na matibabu.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 23,
mwaka huu majira ya saa 4: 45 asubuhi eneo la Mindu, barabara kuu ya Morogoro-
Iringa, Manispaa ya Morogoro, ambapo pikipiki isiyofahamika namba za usajili
iliyokuwa ikiendeshwa na Juma Abasi (18), mkazi wa Mindu kuligonga gari lenye
namba za usajili T 953 AQF aina ya Isuzu Tipper iliyokuwa ikiendeshwa na Joseph
Laurent (28) , mkazi wa Modeco.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo pikipiki hiyo
iliyokuwa ikitokea Mindu Bwawani kuelekea barabara ya Iringa, mwendeshaji wake
alipowaona askari Polisi wawili waliokuwa doria maeneo hayo wakiwa na pikipiki,
aligeuka ghafla na kuingia barabarani bila kuchukua hadhari na kuigonga gari
hiyo iliyokuwa ikitokea Morogoro mjini kuelekea Sangasanga na kusababisha
majeraha kwa mpanda pikipiki huyo.
Kamanda huyo wa Polisi wa mkoa alisema chanzo
cha ajali hiyo ni uzembe wa mwendesha pikipiki huyo kuingia barabarani bila
kuchukua tahadhari.
Hata hivyo alisema ajali hiyo ilishuhudiwa na
askari hao waliokuwa doria na pikipiki maeneo hayo na hivyo walifika eneo la
ajali ili kutoa msaada na katika harakati hizo za kutoa masaada ndipo askari
Koplo Ramadhani alipopigwa na kitu butu kichwani na watu waliotokea eneo hilo
na kuanguka chini.
CHANZO: HABARI LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MOROGORO: 20 MBARONI KWA KUMPIGA ASKARI POLISI.”
Post a Comment