Saturday, April 25, 2015
NYALANDU: TEMBO KUTOWEKA TANZANIA MIAKA 10 IJAYO.
Do you like this story?
Waziri Nyalandu akiendelea kutoa ufafanuzi. |
WAZIRI wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu amesema kama watanzania wasiposhirikiana katika kudhibiti
ujangili wa Tembo waliopo watatoweka kabisa katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
Kauli hiyo ameitoa jana kwenye
mkutano wa ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori
uliofanyika wizarani kwake.
“Uhifadhi kama tunavyoujua,
hautaweza kufanikiwa kama kila mtu kwenye nchi hii atafikiria ni kazi ya
serikali kuu peke yake.
Na vilevile kama kila mtu
atafikiria ni kazi ya wahifadhi peke yao”. alisema Nyalandu kwenye mkutano huo.
Nyalandu alibainisha kuwa,
majadiliano hayo, yatakuwa chachu kubwa ya maendeleo katika wizara hiyo huku
akiwashukuru wadau hao mbalimbali wakiwemo wanahabari kwa kufika kwao, ili
kuangalia suala la uhifadhi kwa mapana yake.
Alisema wakati ujangili wa Tembo
nchini umeshamiri sana, wakati umefika kwa watanzania kuhakikisha kwamba
wanakomesha hali hiyo ili taifa kuendelea kuwa na wanyama wake.
Alisema mathalani Tembo katika
hifadhi ya Selous wamepungua kutoka Tembo 38,975 katika sensa ya mwaka 2009
hadi Tembo 1,384 kwa sensa ya mwaka 2014 na akasema kwa kasi hiyo katika miaka
10 ijayo Tembo Tanzania wataisha kabisa.
“Hili ni muhimu watu wakafahamu,
upana wa hivi vita ni mkubwa kiasi gani na watu wanaohusika ni wengi kiasi gani
ndani na nje ya nchi," alisema Nyalandu akiongeza kuwa mitandao ya
kihalifu imetanda ulimwenguni kote.
Alisema suala la hifadhi halipo
kwa wanyama pekee bali lipo katika upana wote na hata katika misitu.
Alisema ili kukabiliana na
ukatwaji hovyo wa miti kutoka katika misitu ya miombo wanajipanga kuhakikisha
kwamba miombo inayodaiwa kuingizwa nchini kutoka Zambia inakamatwa ili kulinda
miombo iliyopo magharibi ya nchi.
Akizungumzia suala la mifugo na
mbuga zinazopakana nazo amesema kwamba wanaanda rasimu ya kuhakikisha kwamba
kuna mahusiano mazuri kati ya wenye mifugo na hifadhi wakiwa tayari kuyaachia
baadhi ya maeneo kwa lengo la kuhakikisha kwamba wafugaji hawaingizi mifugo yao
katika hifadhi.
Aidha amesema kwamba wanajipanga
namna ya kuhakikisha kwamba hakuna mgongano wa maeneo kati ya wanyama na
binadamu na kwamba wanavijiji wanafundishwa namna ya kuishi na wanyama katika
maeneo yenye mwingiliano mkubwa.
Aidha alisema kwamba meno ya
Tembo kilo 1,763 yalikamatwa mwaka jana na jitihada zinaendelea za kukabiliana
na majangili kwa kutanua mtandao wa kiintelejensia ndani na nje.
Alisema kwa sasa wanamsaka raia
wa China anayeshutumiwa kutorosha nyara za serikali kwa kushirikiana na jeshi
la Polisi la Kimataifa (Interpol).
Kwa nje ya nchi, meno ya Tembo
yaliyokamatwa, Kilo 40 katika miji ya Hong Kong, China.
Aidha alisema watuhumiwa 1,711,
walikamatwa kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana na kesi zao zinaendelea
katika mahakama mbalimbali hapa nchini. Pia silaha 85 zimekamatwa ikiwemo
silaha za kivita ambazo walikuwa wakizitumia mbugani.
Alisema ukichanganya na silaha
zilizokamatwa kwenye operesheni tokomeza, jumla silaha 1,199 zimekamatwa.
Kwa upande wake, Ali Said Mosee
aliyehudhuria mkutano huo kutoka Tanzania Association on Climate Change,
alishauri ushirikishaji wa wadau mbalimbali kutatua migogoro kwenye mipaka ya
mbuga na pia mgongano wa kimaslahi kati ya hifadhi na wanadamu.
Aidha wadau walishauri Wizara
kuhakikisha inapunguza misafara ya wanyama ya kuhamahama kutoka sehemu moja
hadi nyingine ikiwemo kwa kuzalisha miti na mazao yanayopendwa na wanyama hao.
“Wanyama wetu wanatakiwa
wafanyiwe utafiti na kujua nini Nyati anapendelea kula porini, basi wapande
hiyo miti na vyakula vyake kwa ujumla hata kwa Tembo hivyo hivyo.Wapande hiyo
miti hapa hapa kwani hata siye binadamu tunavyovyakula tunavyovipenda, naamini
hata kwa wanyama ni hivyo hivyo, rai yangu ni kuwa tufanye utafiti na kujua ili
kuzuia misafara hii” alisema Ali Said Mosee.
Tanzania inahifadhi za taifa 16
na asilimia 40 ya ardhi ya nchi ni maeneo yaliyohifadhiwa. Kati ya maeneo hayo
yaliyohifadhiwa hadi mwezi uliopita mwaka huu 2015, maeneo 19 yanamilikiwa na
wananchi na yameshasajiliwa. Pia alisema kwamba kuna mapori ya akiba, 28 nchi nzima.
“Watu wengi wanadhani kwamba
misitu yote inamilikiwa na serikali kuu. Ukweli ni kwamba serikali kuu
inamiliki asilimia 35 tu ya misitu ya nchi yetu, misitu mingine yote
inamilikiwa na vijiji, wilaya na watu binafsi asilimia 7. " alibainisha
waziri huyo.
Aliwataka watendaji wa Serikali
za mitaa kukabiliana na changamoto ya kutoweka kwa kasi kwa misitu ili taifa
lisitumbukie katika jangwa.
NA MO BLOG
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ NYALANDU: TEMBO KUTOWEKA TANZANIA MIAKA 10 IJAYO.”
Post a Comment