Tuesday, April 28, 2015

MWENYEKITI WA KIJIJI AKIONA CHA MOTO KWENYE MKUTANO WA HADHARA HUKO LUDEWA NJOMBE


Wananchi wa kijiji cha Mawengi kata ya Mawengi katika wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, wamemlalamikia mwenyekiti wao wa kijiji Bwana Renatho Kahako kwa kula fedha za michango zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya maendeleo huku pia wakimtuhumu kutotoa taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji kwa muda mrefu.

Wananchi hao wametoa malalamiko hayo mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa, Mh. Deo Filikunjombe ambaye naye ameungana na wananchi kumkana mwenyekiti huyo na kudai hafai kuwa kiongozi.

Siku nne za ziara ya Mh.Deo Filikunjombe kuzungumza na wananchi pamoja na kutekeleza shughuli zake mbalimbali za maendeleo wilayani Ludewa, zikamfikisha katika kijiji hiki cha mawengi, hapa bila kuchelea wananchi wakatua malalamiko dhidi ya viongozi wao akiwemo mwenyekiti wa kijiji hicho bwana renatho kahako. 

Hali hiyo ikaibua hasira kwa Mbubge wa jimbo la Ludewa,Mh.Deo Filikunjombe ambaye anakiri kumkabidhi bati 100 mwenyekiti wa kijiji cha mawengi kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi ya mkumbo tangu mwaka 2012 lakini cha kushangaza bati hizo hadi leo hazijafika kwa walengwa.

Katika sakata hilo ambalo nyuma yake likabebwa na minong’ono ya hapa na pale ya wananchi kumkana pia diwani wa kata ya mawengi, Bwana Leodgar Mpambalyoto kwa tuhuma za kuwa mbali na wananchi, diwani huyo akaruka kihunzi futi 100 na kujitetea.

Hata hivyo mbunge huyo amewakabidhi vijana wa kikundi cha cycle star mashine mpya ya kufua UPEPO-COMPRESSOR pamoja na mashine ya kuungia vyuma-welding ambavyo vitasaidia wananchi na wakulima wa mawengi kutengeneza vifaa vyao kwa gharama nafuu.

0 Responses to “MWENYEKITI WA KIJIJI AKIONA CHA MOTO KWENYE MKUTANO WA HADHARA HUKO LUDEWA NJOMBE ”

Post a Comment

More to Read