Tuesday, April 28, 2015

WANANCHI WAVAMIA WIZARA YA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI


Baadhi ya wananchi wa eneo la Mloganzira Kwembe jijini Dar es Salaam wamevamia ofisi za wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi wakishinikiza kulipwa madai yao ya fidia baada ya kupisha mradi wa chuo cha muhimbili na kusababisha shughuli za wizara hiyo kusimama kwa muda.

Wananchi hao wamevamia ofisi hizo huku wakiimba nyimbo mbalimbali zilizokuwa zikishinikiza kulipwa madai yao ambapo wamedai kuwa tangu waondoke kwenye maeneo yao kupisha mradi ni zaidi ya miaka kumi hawajalipwa licha ya Rais kuwaahidi kuwa hawataachwa bila kulipwa.

Kufuatia hali hiyo naibu waziri wa wizara hiyo Mh. Anjela Kairuki amelazimika kutoka ofisini na kuzungumza na wananchi hao ambapo amekutana na wakati mgumu kwani kila alipotaka kuzungumza nao baadhi yao walionekana kutoridhishwa na majibu yake na kuanza kumzomea, na baade aliweza kuwatuliza kwa kuwaeleza kuwa ndani ya siku saba watakwenda eneo husika kuzungumza nao.

Hata hivyo licha ya Mh.Kairuki kutoa kauli hiyo baadhi ya wananchi wamemweleza kuwa wakati wanamsubiri wanarudi kwenye maeneo yao huku wakitishia kusimamisha mradi hadi watakapolipwa fedha zao, ambapo kutokana na hali hiyo polisi walionekana kutanda katika eneo la wizara ya hiyo huku wengine wakiwa na silaha za moto.


0 Responses to “WANANCHI WAVAMIA WIZARA YA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI ”

Post a Comment

More to Read