Thursday, May 7, 2015

WAKULIMA WA MAHINDI MBOZI WALALAMIKIA KUPUNJWA MALIPO YA MAHINDI YAO AMBAYO WALIIKOPESHA SERIKALI KUPITIA NFRA.




Wakulima ambao wameuzia serikali mahindi yao kwa mkopo kupitia wakala wa hifadhi ya chakula ya taifa, NFRA, wilayani mbozi wamelalamika kupunjwa malipo yao baada ya kulipwa kwa kiwango cha chini cha shilingi 350 kwa kilo moja, kinyume na mkataba wa makubaliano ambao unaonyesha kuwa bei ya mahindi hayo ilikuwa ni shilingi 530 kwa kilo moja.
Wakulima hao wamesema kuwa bei ya mahindi ambayo walikubaliana kwa mkataba na NFRA ni shilingi 530 kwa kilo moja ambayo italipwa kwa mkulima atakayefikisha mahindi kwenye ghala la NFRA mjini na shilingi 500 kwa kilo moja kwa mkulima atakayepeleka mahindi yake kwenye maghala ya serikali yaliyo vijijini, lakini wanasikitishwa na hatua ya wao kulipwa shilingi 350 kwa kilo moja jambo ambalo wamedai kuwa ni uonevu mkubwa kwao na kudhoofisha jitihada za wakulima kujikwamua na wimbi la umasikini.

Malalamiko ya wakulima hayo yakawafikia madiwani wa halmashauri ya wilaya ya mbozi ambao wakataka kujua chanzo cha wananchi hao kupunjwa na serikali yao.

Baada ya majadiliano marefu, madiwani hao wakabaini kuwa kuna mkanganyiko mkubwa wa malipo hayo ya wakulima kutokana na baadhi yao kulipwa kupitia kwenye vyama vyao vya ushirika na wengine kulipwa moja kwa moja na Nfra, hivyo wakapendekeza iundwe tume ya kuchunguza suala hilo.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya mbozi, ERIC AMBAKISYE amekubaliana na mapendekezo ya madiwani, lakini akataka tume hiyo ishirikishe uongozi wa mkoa na kutaka baada ya uchunguzi wakulima warejeshewe fedha zao.

0 Responses to “ WAKULIMA WA MAHINDI MBOZI WALALAMIKIA KUPUNJWA MALIPO YA MAHINDI YAO AMBAYO WALIIKOPESHA SERIKALI KUPITIA NFRA. ”

Post a Comment

More to Read