Sunday, July 12, 2015

.DAFTARI LA UBORESHAJI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA KWA MKOA WA DAR ES SALAAM LASOGEZWA MBELE.




Zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura kwa mkoa wa Dar es Salaam limesogezwa mbele hadi Julai 22 mwaka huu.

Uamuzi huo umetokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupokea maombi kutoka kwa wadau mbalimbali walioomba tarehe ya kuanza uandikishaji iliyopangwa kufanyika kuanzia Julai 16 iahirishwe ili kupisha sherehe za Eid-El-Fitr ambazo zinatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe hizo.

Taarifa iliyotolewa na Tume ilisema kuwa kwa kuzingatia umuhimu wa sherehe ya waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na watu wengine Tume imeamua kusogeza tarehe ya kuanza kwa uboreshaji wa daftari hilo hadi Julai 22.

“Tume imezingatia kwa uzito maombi yaliyotolewa na wadau mbalimbali kuhusu kusogezwa mbele tarehe ya uandikishaji uliotakiwa kuanza Julai 16 na badala yake kazi hiyo itaanza rasmi Julai 22 hadi 31 mwaka huu,” ilisomeka taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Tume hiyo, uandikishaji unawahusu wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na wananchi wa kata ya Bunju na Mbweni waliojiandikisha wakati wa majaribio.

Aidha Tume inatoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili wasipoteze haki yao ya msingi ya kidemokrasia.
 HABARILEO.

0 Responses to “.DAFTARI LA UBORESHAJI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA KWA MKOA WA DAR ES SALAAM LASOGEZWA MBELE.”

Post a Comment

More to Read