Tuesday, September 29, 2015
NEC; ALIYETIMIZA MASHARTI ASIZUIWE KUPIGA KURA/.
Do you like this story?
Mungu ni mwema, ndivyo ninavyoanza kusema
katika makala haya, tumshukuru kwa amani tuliyonayo nchini hasa wakati huu
tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Nchi nzima ipo katika mchakato wa kuwapata
viongozi kwa njia ya kura kwa nafasi mbalimbali za kisiasa kupitia vyama vyao
vya siasa, wakati hayo yakiendelea kumekuwepo na taarifa za mchakato huo
kufanyika katika hali ya amani na utulivu katika maeneo mengi nchini, isipokuwa
machache.
Vyama vingi hivi sasa vina wagombea wake
katika ngazi za urais udiwani, ubunge na uwakilishi.
Vyama vyote kwa kiwango kikubwa vimefanikiwa kuwachuja na kuwapata wagombea wao katika maeneo mengi nchini na wadadisi wa masuala ya kisiasa wameeleza kuwepo kwa ishara ya kukua kwa demokrasia ndani ya vyama hivyo na kwa mara ya kwanza tukashuhudia idadi kubwa ya wanachama waliojitokeza kugombea nafasi za uongozi.
Mbali ya sifa hiyo, pia katika maeneo
kulikofanyika kampeni za wagombea mbalimbali, kumeripotiwa kuwepo kwa hali ya
amani na utulivu, licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wanaojitokeza
kusikiliza sera za vyama wakati wagombea wakipeperusha bendera za vyama vyao
kwenye mikutano ya hadhara wanayofanya.
Hali kama hiyo imeripotiwa kujitokeza kwa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
ACT-Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi na vingine
vingi ambavyo vimepata wagombea wake maeneo mengi nchini katika hali ya
utulivu.
Kitendo hicho cha vyama vya siasa nchini
kukamilisha kuwapata wagombea wao katika hali ya amani na utulivu na kuingia
kwenye kampeni kwa zaidi ya mwenzi mmoja sasa ni kitendo kinachopaswa kuungwa
mkono na Watanzania wote kwani kinaashiria mwanzo mzuri wa kufanyika uchaguzi
mkuu kwa amani.
Ingawa vipo viashiria vingine vinavyotajwa na
wadadisi wa masuala ya kisiasa kwamba vinaweza kusababisha uchaguzi mkuu usiwe
huru na wa haki, na hivyo kuashiria uwezekano wa kutoweka kwa amani na utulivu
ikiwemo suala la uandikishaji wapiga kura katika mashine za Biometric Voters
Registration (BVR), lakini hatua ya kampeni kufanyika kwa amani huku
wasikilizaji wa sera wakiwa wengi kwenye mikutano ya vyama vyote vikubwa, ni
jambo linalotia moyo.
Kwa hali hiyo basi ni jukumu la Watanzania
kwa makusudi kuanza kuunga mkono jitihada au vitendo vyovyote vinavyotoa dira
ya uchaguzi mkuu ujao kuwa na utulivu ili kuchochea mazingira ya amani kupanuka
zaidi na kupinga vitendo au viashiria vya kusababisha amani kupotea.
Kama historia inavyosema; Tanzania ni
miongoni mwa nchi chache sana barani Afrika ambayo imekuwa inafanikisha chaguzi
zake katika hali ya amani na utulivu licha ya kuripotiwa kwa baadhi ya matukio
ya vurugu katika maeneo machache.
Mara zote imekuwa ni aghalabu sana kuona
rais, diwani au mbunge wa Tanzania ameingia madarakani kwa kumwaga damu za watu
kama inavyotokea kwa baadhi ya nchi barani Afrika na nje ya bara hili.
Kwa mantiki hiyo, basi ni lazima Watanzania
kwa umoja wao wakaungana pamoja katika kuhakikisha kuwa wanaziba mianya
inayoashiria kuzuka kwa vurugu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ili kulifanya
taifa letu kuendelea kusifika duniani kote kuwa ni kisiwa cha amani na utulivu.
Niiombe Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) chini
ya Jaji Damian Lubuva, kutumia vyombo vya habari kuelimisha wapiga kura
taratibu zitakavyokuwa siku ya kupiga kura hasa tukizingatia kuwa kutokana na
foleni kuwa ndefu wakati wa kuandikisha wapiga kura, baadhi ya watu
walijiandikisha sehemu ambazo siyo makazi yao. Kifupi ni kwamba Nec ihakikishe
kila mwenye shahada halali ya kupigia kura siku hiyo, Oktoba 25, mwaka huu
anapiga kura.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “NEC; ALIYETIMIZA MASHARTI ASIZUIWE KUPIGA KURA/.”
Post a Comment