Friday, September 25, 2015

WATU 41 WAKAMATWA VURUGU ZA KISIASA MBEYA.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Ahmed Msangi


WATU 41 ambao ni wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa vilivyopo ndani ya Mkoa wa Mbeya, wanashikiliwa na polisi kwa makosa mbalimbali likiwemo la kuchana mabango ya wagombea pamoja na bendera za vyama hivyo.

Watu hao, walikamatwa hivi karibuni katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi  zilizoanza rasmi hapa nchini Agosti 22 hadi September 22 mwaka huu katika Mkoa wa Mbeya.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema katika kipindi hicho matukio 30 ya uvunjifu wa amani kipindi hiki cha kampeni  yameripotiwa kutokea katika Wilaya Mbalimbali za mkoa wa Mbeya.

Alisema, katika matukio hayo jumla ya watu 41 wamekamatwa kati yao wanaume ni 32 na wanawake wapo tisa.
“Kati ya matukio hayo yote, tukio moja mtuhumiwa Amani John, alipatikana na hatia na amelipa faini ya shilingi 30,000  huku kesi nane zipo mahakamani katika hatua mbalimbali,”alisema Msangi.

Aidha, Msangi alisema kuwa kesi tatu majarada yake yapo katika ofisi ya mwanasheria wa serikali kwa ajili ya kuandaa mashitaka na kesi 19 bado zipo chini ya upelelezi.

Hata hivyo, alisema kuwa makosa yaliyoripotiwa ni pamoja na kuchana mabango ya wagombea kwa ngazi ya udiwani, Ubunge na urais kesi 17, shambulio kesi 3, kung’oa bendera kesi 2, kuharibu mali kesi 2 kufanya fujo kesi 01, kujeruhi kesi 01, kutishia kuua kwa maneno kesi 01, kuingilia mkutano wa kampeni kesi 01, kupigana hadharani kesi 01 huku kesi ya wizi ikiwa moja.
Mwisho.

0 Responses to “WATU 41 WAKAMATWA VURUGU ZA KISIASA MBEYA.”

Post a Comment

More to Read