Tuesday, November 24, 2015

BOT YAFUNGUA DIRISHA LA CHENJI ZA SARAFU




Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Martin Kobelo amesema benki hiyo imeanzisha dirisha la utoaji wa chenji za sarafu ili kukidhi mahitaji ya ombi la wananchi kutaka huduma hiyo itolewa.

Hivi karibuni sarafu za Sh500, 200, 100 na 50 zimeeendelea kuadimika katika mzunguko wa fedha hali inayochangia usumbufu kwa wafanyabiashara na watu wengine.
Kobelo alisema dirisha hilo litafanya kazi kwa miezi sita ya jaribio la awamu kwa lengo la kuangalia kama hitaji la sarafu hizo litakwisha au litaendelea kuwapo.

“Tumepata malalamiko mengi sana na watu wamekuwa wakipata hasara katika ‘transaction coast’ (gharama ya ubadilishaji wa fedha) imefikia hatua hivi sasa ili upate chenji ya Sh800 unapaswa kutoa Sh1,000.

Alisema tatizo linatokana na idadi kubwa ya wananchi kutokuwa wateja wa benki na wengine kutojua uwapo wa haki ya kupatiwa chenji bure bila kutozwa gharama.

Akizungumzia idadi ndogo ya matawi ya BoT yanayotoa huduma hiyo, Kobelo alisema kila mkoa una tawi linalotoa huduma hiyo kikanda.

Uamuzi huo wa BoT unatazamiwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa chenji katika utoaji huduma za ununuzi na uuzaji wa bidhaa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mbali na hatua hiyo, biashara ya chenji imeonekana kushika kasi zaidi na kupata soko kwa wasafirishaji wa abiria hususan daladala, ambazo zina uhitaji mkubwa wa sarafu hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na BoT juzi, inaeleza kuwa huduma hiyo ya ubadilishaji wa noti kwa sarafu ya Sh500,100,200 na 50 utakuwa ukitolewa na ofisi ya makao makuu Dar es Salaam na katika matawi yake ya mikoa ya Arusha, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Zanzibar. “Huduma hiyo itakuwa ikitolewa mara mbili kwa wiki, Jumanne na Alhamisi kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.Source Mwananchi Online

0 Responses to “ BOT YAFUNGUA DIRISHA LA CHENJI ZA SARAFU”

Post a Comment

More to Read