Thursday, November 12, 2015

KAULI Y MH MEMBE BAADA YA RAIS MAGUFULI KUFUTA SAFARI ZA NJE




Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amempongeza Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kwa kupiga marufuku safari za nje ya nchi, akisema mawaziri na watendaji wa Serikali walikuwa wakigongana angani na ndege utadhani Tanzania ilikuwa ikiwaka moto.


Mbunge huyo wa zamani wa Mtama alisema uamuzi huo utaokoa fedha nyingi za Serikali na kumtaka Rais kushusha rungu hilo hadi kwenye mashirika.


Wakati Membe akieleza hayo, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue alisema kila safari ya nje ina gharama yake na kila safari itakayofutwa zitapatikana fedha kusaidia masuala mengine ya maendeleo katika jamii.


Juzi, Dk Magufuli alipiga marufuku safari za nje ya nchi kwa watendaji na kwamba shughuli ambazo wangekwenda kuzifanya, kuanzia sasa zitahitaji kibali kutoka kwake au zitafanywa na mabalozi wa Tanzania walioko katika nchi husika.


Jana Membe alisema:


"...Tulikuwa tunagongana huko hewani utadhani huku nyumbani kunaungua moto. Tunapobaki huku ndani tunaokoa hela nyingi na nina hakika (Dk Magufuli) ataingilia hata kwenye mashirika. Kuna wakuu wao wanasafiri kila siku, nina hakika wataguswa katika hili. Lazima kuziokoa pesa za kufanyia shughuli nyingine mimi naunga mkono mia moja kwa mia hili?


Alisema kitendo cha Rais Magufuli kufuta safari za nje hakina maana kwamba uhusiano wa Tanzania na nchi hizo unakufa.


"Hajakataza wageni, wafanyabiashara wa dunia wala wawekezaji kuja Tanzania, hata wawekezaji hawawezi kukataa kuja Tanzania waache gesi, dhahabu, almasi au tanzanite.?


Alisema wapo watu wanaodhani kuwa kauli ya Rais Magufuli itamhusu hadi Waziri wa Mambo ya Nje,


"... atakwenda nje maana ukishamuita waziri wa mambo ya nje lazima aende nje. Dk Magufuli hawezi kusema hivyo. Hutasikia amekatazwa maana ndiyo wizara yenyewe na inashughulika na dunia."


Alisema kauli hiyo pia haina maana kwamba Wizara ya Mambo ya Nje imefutwa kwa kuwa balozi za Tanzania zilizopo nje zipo chini ya wizara hiyo.


chanzo:matukiodaima.co.tz

0 Responses to “KAULI Y MH MEMBE BAADA YA RAIS MAGUFULI KUFUTA SAFARI ZA NJE”

Post a Comment

More to Read