Tuesday, November 10, 2015

MIKOPO VYUO VIKUU: MADENTI ‘WAMBANA’ RAIS MAGUFULI MLANGO WA HAZINA




Yadaiwa baadhi ya wanafunzi wanalala Kituo cha Mabasi Ubungo, gesti! Washinda njaa, wajiuza
Mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini imekuwa ni kero kufuatia waliopewa mamlaka ya kusimamia kushindwa kusimamia kwa muda unaotakiwa, jambo linaloleta usumbufu kwa wahusika.

Uchunguzi wa safu hii umebaini kuwa tatizo hili limekuwa likijitokeza kila mwaka na hakuna mwenye uchungu wa kulitatua.Kutokana na usumbufu huo uliojitokeza kwa vyuo vingi nchini, baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Mbeya na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamelalamikia kitendo cha kutopewa mikopo yao na serikali.

Viongozi wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) wamedai uwingi wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza ambao hawajapewa mikopo hiyo ya fedha za elimu unatisha.

KULALA VITUONI
Yapo madai kuwa kwa sasa hali ni mbaya kiasi kwamba baadhi yao wanalala katika Kituo cha Mabasi Ubungo, gesti, wanashinda na njaa huku wengine wa kike wakiwa wanajiuza kwani walivyotarajia kupokelewa na kupewa mikopo imekuwa ni tofauti.

Mwandishi wetu alifika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata malalamiko mengi kuhusiana na hali halisi ya mateso wanayoyapata baadhi ya wanafunzi kutokana na kukosa mikopo hali iliyosababisha wengine kuamua kurudi makwao na kile walichodai kwamba huwezi kusajiliwa chuoni hapo bila kupata mikopo.

RAIS WA WANAFUNZI ANENA
Rais wa wanafunzi chuoni hapo, Ahadi Kitaponda akiwa na makamu wake, Irene Ishengoma, alisema kwamba hali ni mbaya kwani mkopo kwa wanafunzi mwaka wa kwanza ilibidi wapate wanafunzi zaidi ya 6,000 lakini waliopata ni 684 tu.

Rais huyo aliendelea kusema kwamba kutokana na hali hiyo waliojisajili ni wachache kutokana kuwa wengi wanategemea mikopo kwa ajili ya kulipia ada ya chuo. “Wanafunzi walianza kuripoti hapa tangu mwezi uliopita. Kutokana na hali hii wengine wamekata tamaa na kurudi makwao huku baadhi yao ndiyo wanalala katika mazingira mabaya kama vile kwenye Kituo cha Mabasi Ubungo.

“Hali hii inaleta kishawishi kwa baadhi ya wanafunzi wa kike kujiuza ili waweze kujikimu au kukabiliana na maisha,” alisema kiongozi huyo.Hata hivyo, rais huyo aliendelea kusema kwamba kutokana na hali hiyo alilazimika kumtuma Waziri wa Mikopo wa Daruso, Shitindi Venance na viongozi wengine kwenda Wizara ya Elimu na kuonana na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Dk. Jonathan Mbwambo ambaye alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuahidi kulishughulikia.

Anasema amefikia hatua ya kumuona Dk. Mbwambo baada ya kutopatikana kwa katibu mkuu ofisini kwake.
Hata hivyo, walimuachia taarifa katibu wake, Martini Muhando kisha kwenda Wizara ya Fedha na kukutana uso kwa uso mlangoni na Rais Dk.John Mgufuli wakati akitoka wizarani hapo ambapo ‘walimbana’ na kumweleza tatizo hilo.
“Rais Magufuli aliwajibu kuwa wasubiri amchague Waziri wa Fedha na kuahidi kutatua malalamiko yetu.

“Hali ikizidi kuwa mbaya kwa kukosa mahali pa kuwapeleka wanafunzi hawa wala jinsi ya kupata malazi tutaitisha mkutano na kutoa tamko letu kama wanafunzi,” alisema rais huyo wa wanafunzi.Uchunguzi unaonesha kwamba tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa hapa nchini ni kero kubwa hali inayosababisha wanafunzi kuandamana kwa lengo la kufikisha ujumbe lakani wamekuwa wakikabiliana na polisi na kuzua ghasia ambapo wamekuwa wakipigwa virungu na kumwagiwa maji ya kuwasha.

CHUO KIKUU MBEYA NAKO
Wanafunzi wengine wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Mbeya walisema wao hata mmoja hajapewa mkopo huo.“Bado wiki moja tunatakiwa kuripoti chuoni na usipokwenda utatakiwa kila siku ambayo haupo ulipe shilingi 20,000,” alisema mwanafunzi mmoja wa mwaka wa kwanza wa Mbeya ambaye hakutaka jina lake kuandikwa kwa kuwa siyo msemaji.

Viongozi wenye dhamana ya kusimamia mikopo ya wanafunzi wanaonekana kushindwa kutatua tatizo hilo licha ya serikali kutenga fedha hizo.

0 Responses to “ MIKOPO VYUO VIKUU: MADENTI ‘WAMBANA’ RAIS MAGUFULI MLANGO WA HAZINA”

Post a Comment

More to Read