Tuesday, November 17, 2015

MKWASA AELEZA MBINU ATAKAZOTUMIA LEO KUIMALIZA ALGERIA KWAO




Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania jana kilifanya mazoezi yake ya mwisho kuelekea kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya timu ya Algeria utakaochezwa leo majira ya saa 3 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Mustapher Tchaker uliopo kwenye mji wa Blida, Algeria.

Kuelekea mchezo huo, Yahaya Mohamed amezungumza na kocha mkuu wa Stars Charles Boniface Mkwasa kuhusiana na maandalizi ya kuelekea mchezo huo.

“Mechi hii tumejipanga vizuri zaidi kwasababu mechi ya kwanza ilikuwa mechi yetu lakini bahati mbaya hatukuweza kupata matokeo mazuri zaidi lakini najua mechi hii itakuwa ngumu wao wako nyumbani wana mbinu nyingi. Nimepata taarifa kuwa baada ya kufanya worm-up huwa wananyunyizia maji mengi uwanjani lakini sisi tumejipanga kwa lolote lile na kama watanyunyizia maji tutawaeleza wachezaji wajipange ni jinsi gani wataweza kucheza”, amesema Mkwasa.

Mkwasa amesema kutakuwa na mabadiliko kidogo ya kimbinu lakini mambo mengine yatabaki vilevile, huku akisisitiza kutaka kuhakikisha wanamiliki eneo la kiungo pamoja na ulinzi pamoja na kuzitumia vizuri nafasi zitakazopatikana.

“Tutakuwa na mabadiliko kidogo lakini si sana kwasababu approach ni ileile na falsafa ni ileile kwamba tujaribu kumiliki kwenye upande wa kiungo na ulinzi na tutumie nafasi vizuri. Kwasababu hata wao timu yetu wameiona inawezekana kabla hatujacheza nao walikuwa wanatudharau sana, lakini kwasababu wameshatuona wanaweza wakacheza kwa tahadhari kubwa na wasiwasi na kutupa sisi fursa ya kufanya vizuri”.

Kuelekea mchezo wa leo, Stars inaweza ikamkosa winga wake Farid Musa ambaye alimaliza mchezo wa jijini Dar es Salaam akiwa na maumivu kwahiyo kunauwezekano mchezaji huyo akawepo au asiwepo kwenye mchezo huo.

0 Responses to “MKWASA AELEZA MBINU ATAKAZOTUMIA LEO KUIMALIZA ALGERIA KWAO”

Post a Comment

More to Read