Wednesday, November 11, 2015

TFDA YAJA NA MBINU MPYA YA KUZUIA VIPODOZI FEKI MBEYA


Meneja wa Mamlaka hiyo nyanda za juu kusini Rodney Alananga



NA SAMWEL NDONI MBEYA
MAMLAKA ya chakula na dawa (TFDA) kanda ya nyanda za juu kusini imekuja na mbinu mpya ya kudhibiti matumizi ya vipodozi vyenye viambata sumu na vilivyopigwa marufuku nchini inayoitwa ‘oparesheni tokomeza vipodozi vyenye viambato sumu’.

Akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Azimio, Chuo cha Veta na Chuo cha Ustawi wa Jamii Uyole jijini Mbeya kwa nyakati tofauti, Meneja wa Mamlaka hiyo nyanda za juu kusini Rodney Alananga alisema kuwa kampeni hiyo inalenga kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo mbalimbali kuhusu madhara ya matumizi ya vipodozi hivyo.

Alananga amesema kuwa wameamua kuja na kampeni hiyo kabambe baada ya kubaini kuwa kuna baadhi ya wafanya biashara ambao wanaendelea kuingiza vipodozi hivyo kwa njia za panya licha ya jitihada za kuvikamata na kuviteketeza kwa moto hivyo wameamua kutoa elimu kwa makundi kushawishi wasinunuwe na kuvitumia.



Aliyataja baadhi ya madhara ya vipodozi hivyo kuwa ni pamoja na kusababisha kuharibu uzio wa ngozi na kupenya hadi kwenye damu, hivyo kuwa na uwezekano wa watumiaji kupata kansa ya Ngozi, damu, mapafu, figo, muwasho pamoja na mabaka meupe na meusi.

vile vile alisema kwa  mama mjamzito akitumia vipodozi nyenye viambata vya Zebaki mtoto huzaliwa akiwa na mtindio wa ubingo huku akiongeza kuwa mtumiaji wa vipodozi hivyo akipata jeraha haliponi.

Amesema kuwa Mamlaka hiyo sasa imeanzisha mkakakati kwa wanafunzi wa shule za msingi pamoja na vyuo ili kupanua wigo wa uelewa kuhusu madhara hayo kwa kuwa makundi hayo baadhi yao wameanza kutumia vipodozi hivyo kwa kufahamu ama kutofahamu madhara yake huku akidai kuwa vingine madhara huanza kuonekana baada ya kutumia kwa muda mrefu.

Aliongeza kuwa baadhi ya wafanyabiashara pamoja na  wajasiriamali wamebuni mbinu mpya ya ushawishi kwa watumiaji kuwa vipodozi hivyo vinatengenezwa kwa kutumia mimea ya  asili.

Alievitaja  viambato  kumi na  moja vyenye sumu vilivyopingwa marufuku ambavyo ni Bithionol, Hexachlophene, Zebaki, Vinyl Chloride, Ziconium, Halogenated salicylanilide, Chloroquinenone, Hydroquinone, Steroids, Chroloform, Chlorofluorocaborn, pamoja na Methylene Chloride.
MWISHO


0 Responses to “TFDA YAJA NA MBINU MPYA YA KUZUIA VIPODOZI FEKI MBEYA”

Post a Comment

More to Read