Wednesday, November 11, 2015
JESHI LA POLISI KATAVI LAFANIKIWA KUZIMA NDOA YA WATOTO,BWANA HARUSI ANA MIAKA 17 BIBI HARUSI 14.
Do you like this story?
Jeshi la Polisi
mkoani Katavi limefanikiwa kuzuia kufungwa kwa ndoa iliyohusisha watoto,
muolewaji akiwa na umri wa miaka 14 na muoaji ana umri wa miaka 17.
Kwa mujibu wa
taarifa, bibi harusi ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi
Mwamkulu iliyopo kijiji cha Senta John Mwamkulu, Wilayani Mpanda, mkoani
Katavi, na bwana harusi aliacha shule alipokuwa darasa la tatu.
Mwanafunzi huyo
(14), (jina linahifadhiwa) siku ya harusi alikuwa afanye mtihani wa wilaya,
lakini alikutwa akiwa amevaa shela tayari kwa kufungishwa ndoa ya kimila
nyumbani kwao kwa mahari ya ng’ombe kumi na moja.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema tukio hilo lilitokea juzi
saa saba mchana katika kijiji Senta John Mwamkulu, wilaya ya Mpanda.
Alisema polisi
wakiwa na viongozi wa elimu wa Manispaa ya Mpanda, walienda nyumbani kwao na
kukuta msichana huyo akiwa na shela tayari kufungishwa ndoa kinyume cha sheria.
Alisema jeshi
hilo linamshikilia bwana harusi (jina linahifadhiwa), baba yake bwana harusi
Ntunga Mkubaneja (40) na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwankulu, Raphel
Kweka, anayedaiwa kupewa Sh500,000 ili afute jina la mwanafunzi huyo shuleni.
Akisimulia
tukio hilo, Kamanda Kidavashari alisema wakati mchakato wa kufungwa kwa ndoa
hiyo ukiendelea, mkazi wa kijiji hicho alifunga safari mpaka ofisini kwake na
kutoa taarifa juu ya kuwepo kwa ndoa hiyo kinyume cha sheria.
“Tulipewa
taarifa kuwa kuna mwanafunzi anaozeshwa kinyume cha sheria na harusi yake
inafungwa mchana wa tarehe tisa, mwezi huu. Tulijiandaa tukakubaliana na watu
wa elimu kisha tukaenda kijijini na kukutana na shamra shamra za kumuozesha
mwanafunzi kama tulivyoambiwa,”alisema.
Ofisa Elimu wa
Manispaa ya Mpanda, Vincent Kayombo alisema mwanafunzi huyo alikuwa darasa la
nne na kuwa siku ya harusi yake alitakiwa kufanya mtihani wa wilaya (Mock).
Kayombo alisema
alishangazwa na hatua ya wazazi kuamua kumuozesha mtoto wao wakati akiwa bado
darasa la nne, kwa mahali ya ng’ombe 11 kinyume cha sheria.
Alilitaka Jeshi
la Polisi kufanya utafiti juu ya tuhuma za mwalimu mkuu kuhusika kwenye sakata
hilo, kwa kudaiwa kupokea fedha ili akibainika, hatua za kisheria zichukuliwe
dhidi yake.
“Mleta taarifa
alimtaja mwalimu mkuu kuwa alipewa fedha kuhalalisha mwanafunzi huyu aolewe,
kwa kuwa wapo chini ya vyombo vya sheria haki itatendeka,”alisema Kayombo.
Naye Ofisa
Maendeleo wa Manispaa ya Mpanda, Zena Kapama aliviomba vyombo vya sheria
kuchukua hatua dhidi ya jambo hilo ili kukomesha vitendo vya kuozesha wanafunzi
wakiwa kwenye umri mdogo.
“Tulimkuta
mtoto akiwa amevaa shela tayari kuolewa, alikiri kuwa haikuwa ridhaa yake
kuolewa na ndipo tukafanikiwa kuwakamata bwana harusi, bibi harusi mwenyewe,
baba wa bwana harusi na mama yake bwana harusi huku baba mzazi wa bwana harusi
akikimbia,”alisema.
Akizungumza na
waandishi wa habari msichana huyo aliyenusurika kuolewa, alisema haikuwa ridhaa
yake kuolewa na kijana hiyo.
“Baba
alilazimisha niolewe akidai kuwa shuleni sina akili, nilikataa nikaomba
niendelee kusoma shule kwa sababu elimu itanisaidia nikiwa mkubwa lakini
alikataa. Niliomba niende mjini kuishi kwa baba mkubwa, yote baba alikataa
alichotaka yeye niolewe,” alisema.
Alisema suala
lake la kuolewa lilileta mzozo nyumbani kwao kwa kuwa mama yake hakuwa tayari
mwanaye huyo aolewe akiwa na umri mdogo.
Mama wa
mwanafunzi huyo, Esther Martin alisema binti yake alilazimishwa kuolewa na
kwamba hakuwa na uwezo wa kukataa kwa kuwa tayati mumewe alikuwa amepokea
mahali ya ng’ombe 11.
“Mtoto aliitwa
mbele yangu kulazimishwa aolewe kwa madai hana akili shuleni kwa kuwa hajui
kusoma, alilazimika kukubali tu nilimshauri baba yake asimuozeshe kwa sababu
hata Serikali haitaki, akakataa,”alisema mama huyo.
Baba wa bwana
harusi huyo, Mkubaneja alisema alilipa mahali ili mwanaye amuoe msichana huyo
bila kujua kama alikuwa mwanafunzi.
Kwa upande wake
bwana harusi, ambaye alidai kuishia darasa la tatu alisema aliamua kumuoa
msichana huyo baada ya kumpenda, lakini hakujua kama ni mwanafunzi baada ya
wazazi wa binti huyo kukubali kupokea mahali toka kwa wazazi wake.
Mwalimu Mkuu
Kweka, alikataa kuhusika kumuozesha mwanafunzi huyo, pia alikanusha madai ya
kupokea fedha kutoka kwa baba wa binti huyo.
Alisema taarifa
zote za mwanafunzi huyo ambaye alitakiwa kufanya mtihani wa darasa la nne siku
ya harusi yake ikiwamo namba yake ya mtihani zipo.
“Vielelezo
vyote ambavyo vinamuhusu mwanafunzi vipo likiwamo daftari la mahudhurio,
ninachojua huyu binti ni mtoro wa ‘rejareja’. Sijawahi kuchukua kiasi chochote
cha hela kwa mzazi wake, wala ndugu yake wala mtu yeyote anayefanana naye,”
alisema Mwalimu huyo.
Mtetezi wa
masuala ya kijinsia nchini, Gemma Akilimali alilitaka jeshi la polisi
kuhakikisha wahusika wanapelekwa mahakamani, ili sheria ichukue mkondo wake.
“Tuwashukuru
waliojitahidi kumuokoa mtoto huyo kabla hajaolewa, ombi letu wanaharakati ni
kwamba kesi hiyo isiishie hewani, wazazi waliopokea na kutoa mahali lazima
wachukuliwe hatua za kisheria ili iwe fundisho,”alisema.
Alisema ikiwa
jamii itaendelea kutoa ushirikiano kwa kufichua wazazi wenye tabia ya kuozesha
wasichana wenye umri mdogo, tatizo hilo litapungua.
Akilimali
aliongeza kuwa mwanafunzi huyo anatakiwa kurejea shuleni ili aendelee na masomo
yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “JESHI LA POLISI KATAVI LAFANIKIWA KUZIMA NDOA YA WATOTO,BWANA HARUSI ANA MIAKA 17 BIBI HARUSI 14.”
Post a Comment