Wednesday, November 11, 2015
YULE BIBI HARUSI ALIYEMKIMBIA MUMEWE SIKU YA HARUSI APATIKANA....SOMA HAPA KUJUA ALIPOKUWA AMEKIMBILIA.
Do you like this story?
Bibi harusi Doroth Msuya( Kulia ) |
Bibi harusi
Doroth Msuya aliyetoroka saluni akipambwa saa tatu kabla ya kufungwa kwa harusi
yao na kumwacha solemba bwana harusi, Joseph Machange amepatikana jijini
Arusha.
Polisi mkoani
Kilimanjaro imesema binti huyo hakutekwa nyara kama ambavyo wanafamilia walitoa
taarifa Kituo cha Polisi Himo.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema jana kuwa uchunguzi
uliofanywa umethibitisha kuwa bibi harusi huyo hakuwa ametekwa nyara.
“Polisi
walifungua jalada la uchunguzi na ilibainika kuwa taarifa za kutekwa zilizokuwa
zimetolewa hazikuwa na ukweli, bali aliondoka kwa kupanda pikipiki,” alisema.
Kamanda Ngonyani
alisema uchunguzi huo ulibaini kuwa wakati akipambwa, aliomba kwenda kujisaidia
na baadaye kuomba apelekewe kanga na ‘tishu’ lakini akatumia mwanya huo
kuondoka,” alisema.
Alisema
uchunguzi huo umebaini kuwa baada ya kupanda pikipiki ilimpeleka hadi kituo cha
mabasi na alimlipa dereva wa bodaboda kisha alipanda gari la abiria
lililompeleka hadi mjini Moshi.
Tukio hilo
lilitokea Jumamosi iliyopita saa 6.30 mchana eneo la Lole huko Mwika, Moshi
wakati bibi harusi huyo alipotoroka saluni akimwacha mpambe wake akiendelea
kupambwa.
Ndoa hiyo
ilikuwa ifungwe saa tisa alasiri katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Usharika wa Lole Dayosisi ya Kaskazini na baadaye sherehe
ingefanyika katika Ukumbi wa Mamba Complex.
Habari
zilizopatikana jana kutoka kwa familia ya Machange, zilieleza kuwa Doroth
alipatikana juzi baada ya kuonekana akiweweseka, kisha akapelekwa hospitali ya
Seliani kwa matibabu.
Ndugu wa karibu
wa familia ya Machange ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alisema kulikuwa na
kikao kilichokuwa kikiendelea kati ya familia ya Machange na Msuya.
“Jana (juzi)
tulipigiwa simu na kuelezwa kuwa Doroth amepatikana Arusha lakini yuko kama
hajielewielewi na hajui nini kimetokea,” alisema.
Habari zaidi
kutoka ndani ya familia hiyo, zinadai kuwa bibi harusi huyo alikuwa ametaka
harusi hiyo iahirishwe na ombi hilo alilitoa zaidi ya mara 10 bila kueleza
sababu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “YULE BIBI HARUSI ALIYEMKIMBIA MUMEWE SIKU YA HARUSI APATIKANA....SOMA HAPA KUJUA ALIPOKUWA AMEKIMBILIA.”
Post a Comment