Friday, December 4, 2015

MBEYA CITY FC YANASA WAWILI, WENGINE WATATU KUFUATA




Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam 
KLABU ya kizazi kipya, Mbeya City FC imefanikiwa kuwasaini wachezaji wawili hadi sasa kati ya watano ambao wamepanga kuwaongeza katika usajili huu wa dirisha dogo. City ambayo ilimaliza katika nafasi ya tatu katika msimu wake wa kwanza ligi kuu bara ( 2013/14) na nafasi ya nne msimu uliopita imeonekana kushuka kiwango huku kuondoka kwa wachezaji zaidi ya kumi msimu huu kukichangia timu hiyo kuanza msimu huu kwa matokeo mabaya.

Ikiwa katika nafasi ya 11 huku ikiwa imekusanya pointi tisa (9) tu katika michezo kumi, Mbeya City imekusudia kuimarisha kikosi chao. Tayari wamemsaini mlinzi wa kati, Tumba Sued kutoka Coastal Union ya Tanga ili kuchukua nafasi ya Juma Nyosso ambaye amefungiwa kucheza mpira kwa miaka miwili.

Mshambuliaji wa zamani wa Kagera Sugar, AFC Arusha, Simba SC na Mtibwa Sugar, Abdallah Juma pia amesaini mkataba wa kujiunga na timu hiyo ya Mbeya. City itacheza na Mtibwa mwishoni mwa wiki ijayo katika uwanja wa Sokoine. Tayari wapo kambini kwa wiki ya pili sasa na wamedhamiria kufanya vizuri zaidi baada ya ligi kuanza tena baada ya kusimama kwa miezi karibia miwili.

“Tunaendelea kuzungumza na wachezaji wengine ambao mwalimu amewapendekeza kuwasajili. Hadi sasa tumeshamalizana na Tumba Sued na mshambuaji Abdallah Juma ambaye alikuwa Toto Africans. Lengo ni kuongeza wachezaji watano kufikia tarehe 15 mwezi huu siku ambayo usajili utafungwa”, anasema Emmanuel Kimbe katibu mkuu wa timu hiyo.

0 Responses to “MBEYA CITY FC YANASA WAWILI, WENGINE WATATU KUFUATA”

Post a Comment

More to Read