Friday, December 4, 2015

YANGA YAANZA KUPIGA CHINI WACHEZAJI WAKE, TAYARI MMOJA ATOSWA KIPINDI HIKI CHA DIRISHA DOGO…JE, KUNA WENGINE YATAWAKUTA?




Mlinda mlango wa mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara klabu ya Yanga amejikuta hayupo kwenye hesabu za benchi la ufundi kwa ajili ya wachezaji ambao wanahitajika kukitumikia kikosi hicho cha Jangwani.
Mudathir Khamis ametupiwa virago vyake kutoka klabu ya Yanga na tayari amesharejea Zenj kama mchezaji huru na anaweza kujiunga na timu yoyote.

Baada ya kuzagaa taarifa hizo kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa mlinda mlango wa Yanga Mudathir Khamis ameachwa, mtandao huu leo umemtafuta mchezaji huyo na kusema kuwa amependelea aongee na kocha wake wa zamani wa KMKM Ali Bushir na kumpa taarifa hizo ambapo tayari amemuonesha barua yake.

Tukamtafuta kocha Ali Bushir na kuthibitisha kuwa kweli Muda ameachwa na kikosi cha Yanga.

“Nikweli Mudathir ameachwa na Yanga na mimi leo asubuhi kaniletea barua hiyo ambayo kasaini katibu wa Yanga, nimeipitia barua hiyo ya kusitisha rasmi mkataba na Yanga na kumuwachia awe huru kwenda klabu yoyote, barua hiyo imeandikwa tarehe 21 November ikisema kuwa Mudathir si mchezaji tena wa Yanga”, amesema kocha Bushir.

Aidha kocha Bushir amesema wachezaji lazima wawe makini pale wanaposaini mikataba na timu akiwataka kutafuta wanasheria ambao watawasimamia ili wasije kukosa haki zao za msingi pindi yanapotokea matatizo mengine ya kusitishwa mikataba yao kiholela.

Yanga imeamua kusitisha mkataba na mchezaji huyo mkataba ambao ulikuwa unamalizika mwezi Mei, 2018.

0 Responses to “YANGA YAANZA KUPIGA CHINI WACHEZAJI WAKE, TAYARI MMOJA ATOSWA KIPINDI HIKI CHA DIRISHA DOGO…JE, KUNA WENGINE YATAWAKUTA?”

Post a Comment

More to Read