Thursday, June 30, 2016
GESI ILIYOGUNDULIWA TANZANIA YAZUA MJADALA MZITO.
Do you like this story?
Wakati
Rais John Magufuli akiungana na Watanzania wengine wanaofurahia kugunduliwa kwa
gesi ya helium nchini, baadhi ya wataalamu wa miamba wameshauri uchunguzi zaidi
ufanyike ili kuthibitisha uwepo wa kiasi hicho.
Juzi, kulikuwa
na taarifa za watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Oxford na kile cha Durham kwa
ushirikiano na wataalamu wa madini kutoka Norway kuwa wamegundua uwepo wa
takriban futi 54 bilioni za ujazo za hifadhi kubwa zaidi duniani ya gesi adimu
zaidi ya helium katika Bonde la Ufa, Kusini mwa Tanzania.
Katika
ukurasa wake wa Tweeter, Dk Magufuli alisema ni jambo la kumshukuru Mungu huku
akiwataka wachumi, wanasheria na Watanzania kwa ujumla kujiandaa.
“Tunamshukuru
Mungu Tanzania tumegundua gesi aina ya helium, wito wangu kwa wachumi,
wanasheria na Watanzania wote kwa ujumla tujipange. Ugunduzi huu utuelekeze
kujipanga hasa katika eneo la mikataba yetu ili rasilimali hii adimu isaidie
kuujenga uchumi wetu,” alisema.
Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikaririwa akithibitisha ugunduzi
huo na kusema Serikali itaitumia gesi hiyo vizuri.
Hata
hivyo, akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Miamba
(Geological Survey of Tanzania), Profesa Abdulkarim Mruma alisema hawakushiriki
kwenye utafiti huo, hivyo ni mpaka wafanye utafiti wao kuthibitisha.
“Kwanza
tulikuwa na mradi wa kutafuta helium na Wajerumani na tuliainisha maeneo
yanayoweza kupatikana. Kwa hiyo hao watatifi walikuja kufuatilia maeneo
tuliyoyaweka, ila hatukwenda nao,” alisema.
“Unajua
mara nyingi watafiti wa madini huwa wana tabia ya kutaja viwango vikubwa vya
upatikanaji wa madini ili kuongeza hisa za kampuni zao kwenye masoko ya madini.
Kwa hiyo tutafuatilia kwa kuchimba ili kuhakikisha kama kweli hicho kiwango
walichosema kipo. Kama hakipo tutawaeleza,” alisema
Profesa Mruma.
Alisema
gesi ya helium imekuwa ikipatikana kwa kiasi kidogo nchini tangu wakati wa
ukoloni, lakini ugunduzi wa sasa ni mkubwa kidunia.
Mkurugenzi
wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk James Mataragio alisema
hawana taarifa rasmi ya ugunduzi huo, hivyo hawezi kusema Taifa litafaidikaje.
“Tangu
jana (juzi) tumeona vyombo vya habari vimeandika kuhusu gesi hiyo. Ukweli ni
kwamba sijapokea taarifa rasmi kuhusu ugunduzi huo. Uchimbaji wa gesi ya helium
ni tofauti kidogo na gesi nyingine, ni mpaka ithibitishwe kwanza na wataalamu
kama ipo kweli ndipo tujue tutafaidikaje,”
alisema.
Mkuu wa
Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Elisante Mshiu alisema kama
kweli kiasi hicho cha gesi kipo, Tanzania itakuwa na gesi hiyo mara mbili
kuliko inayopatikana kote duniani.
Dk Mshiu
alisema gesi hiyo inayopatikana maeneo mbalimbali duniani ina mita za ujazo 25
bilioni, hivyo iliyopo Tanzania ni mara mbili yake.
Akizungumza
kupitia mtandao wa ABC, mmoja wa wanasayansi Profesa Chris Ballentine kutoka
Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza alisema gesi hiyo iliyogunduliwa inaweza
kutumika kwa zaidi ya miaka 20 ijayo.
Profesa
Ballentine anayefanya kazi na kampuni ya Norway ya kutafuta helium, alisema ni
mara ya kwanza kuitafuta helium na kuipata kwani mara nyingi hupatikana kwa
bahati tu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ GESI ILIYOGUNDULIWA TANZANIA YAZUA MJADALA MZITO.”
Post a Comment