Monday, July 4, 2016
AGIZO LA KUZUIA UVUTAJI WA SIGARA NA MATUMIZI YA SHISHA,TUMBAKU KATIKA MAENEO YA UMMA
Do you like this story?
Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inampongeza Mheshimiwa Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kupiga marufuku matumizi ya Shisha
na uvutaji wa Sigara hadharani kama afua ya kupunguza madhara ya tumbaku na
madawa ya kulevya katika jamii.
Uchunguzi
wa kitalaam uliofanyika umebaini kuwa Shisha ina madhara kwa afya ya watumiaji
hasa vijana na watoto. Watumiaji wa Shisha wanatumia kiwango kikubwa cha
tumbaku kwa muda mfupi, hali inayoongeza madhara yatokanayo na tumbaku kama
vile: – Saratani, Magonjwa ya Mapafu, Kibofu cha mkojo, Tezi dume, Koo, Mdomo
na Kiywa, Ngozi, Ini, Ubongo.
Pia
imebainika kwamba matumizi ya Shisha huambatana na kuongezewa dawa nyingine za
kulevya na hivyo hufanya watumiaji wa Shisha kupata uraibu wa dawa za kulevya.
Matumizi ya dawa hizo za kulevya ni kosa la jinai.
Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kurejea na
kusisitiza agizo lake la tarehe 12 Machi 2015 la kuzuia matumizi ya sigara na
matumizi ya bidhaa za tumbaku katika maeneo ya umma
Inakumbushwa
kwamba agizo hili limezingatia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za
Tumbaku, Sura ya 121 T.L 2002, ya Sheria za Tanzania kipengele cha 12 (1)
ambacho kinakataza matumizi ya Tumbaku katika Maeneo ya Umma.
Madhumu ya
Agizo hili ni kuilinda Jamii kwa ujumla kutokana na madhara yatokanayo na moshi
wa sigara. Wizara inawakumbusha wananchi wanaotumia bidhaa za tumbaku kupunguza
au kuacha kabisa matumizi ya tumbaku. Aidha, agizo hili linaijumuisha jamii
yote katika kubaini madhara ya tumbaku na umuhimu wa kuzuia matumizi ya tumbaku
katika maeneo ya kazi na maeneo yote ya umma.
Agizo hili
linawahusu wananchi wote nchini wanaopata huduma katika maeneo ya umma kama
ilivyotafsiriwa na sheria husika.
Matumizi
ya tumbaku hayaruhusiwi katika maeneo yote ya umma. Maeneo haya yanajumuisha
ofisi zote za Serikali na tasisi zake zote, watu binafsi, vyuo, vituo vya
huduma za Afya zikiwemo Hospitali, vituo vya Afya na zahanati, vituo vya
usafiri wa Anga, Mabasi, bandari na treni, sehemu za mikutano, mapumziko,
bustani na fuko za maji,sherehe,michezo,masoko,maduka makubwa pamoja na sehemu
za kuabudu.Na kwa mtu yeyote anayeendesha shughuli katika maeneo ya umma
analazimika kutenga eneo maalum kwa ajili ya wavuta sigara.
Kwa kuwa
Mhe. Waziri mwenye dhamana na masuala ya Afya nchini ameona hatari hii ya
Uvutaji wa sigara na utumiaji wa bidhaa za tumbaku kwa afya ya Wananchi,
kuanzia leo tarehe 4/7/2016 matumizi ya Shisha nchini yamepigwa marufuku kwa
wote wanaojihusisha na matumizi hayo, na kwa wafanyabiashara wote
wanaojihusisha na upatikanaji wa Shisha nchini
Hivyo
basi, kwa agizo hili katika maeneo yote nchini ambako matumizi ya Shisha
hufanyika ni marufuku matumizi hayo kuendelea kutumika.
Aidha
vyombo vya Dola na mamlaka husika vinahimizwa kusimamia kwa ukamilifu katazo
hili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “AGIZO LA KUZUIA UVUTAJI WA SIGARA NA MATUMIZI YA SHISHA,TUMBAKU KATIKA MAENEO YA UMMA”
Post a Comment