Thursday, July 14, 2016

WAZIRI MKUU MPYA WA UINGEREZA ATANGAZA BARAZA LAKE JIPYA LA MAWAZIRI




Waziri mkuu mpya wa Uingereza, Theresa May amemteua Boris Johnson kuwa waziri wa Mambo ya Nje na Philip Hammond kuwa Waziri wa Fedha wa nchi hiyo.

Aidha Amber Rudd ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Michael Fallon ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi.

Waziri Mkuu huyo mpya wa Uingereza amesema kuwa serikali yake haitanaswa na mtego wa kuwasikiliza watu walio wachache na kusahau wananchi wa kawaida. Theresa May anakuwa waziri mkuu wa 13 kuwahi kuiongoza Uingereza katika enzi ya Malkia Elizabeth wa pili.

Hapo jana waziri mkuu aliyetangaza kujiuzulu hivi karibuni, David Cameron alihutubia kwa mara ya mwisho Bunge la Uingereza na kujibu maswali ya wabunge wa Bunge hilo na baadaye aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Malkia Elizabeth wa Pili kwenye Kasri lake lililopo huko Buckingham.

Malkia amemtaka Bi May kuunda serikali ikiwa ni historia ya pekee kwa Uingereza kupata kiongozi wa pili mwanamke baada ya Margaret Thatcher.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya (EU) wameitaka serikali ya Uingereza kuharakisha mchakato wa kujitoa rasmi katika umoja huo, lakini May amedokeza kuwa hatauharakisha mpango huo mashuhuri kwa jina la Brexit.

Changamoto kubwa inayomkabili Waziri Mkuu huyo mpya wa Uingereza ni pamoja na kuizuia Scotland inayounga mkono Umoja wa Ulaya dhidi ya kuitisha kura ya uhuru wake ili kubakia katika EU na kuimarisha mahusiano mapya ya kibiashara na kidiplomasia ili kujiandaa kwa hali ya baadaye ya baada ya kujiondoa katika umoja huo.

0 Responses to “ WAZIRI MKUU MPYA WA UINGEREZA ATANGAZA BARAZA LAKE JIPYA LA MAWAZIRI”

Post a Comment

More to Read