Friday, July 1, 2016
WAZIRI MKUU:SERIKALI ITATOA WARAKA JUU YA UKUSANYAJI MAPATO KUPITIA MAWAKALA.
Do you like this story?
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Halmashauri zitaelekezwa kwa waraka ni vyanzo vipi
vitahitaji kutumia wawakala wa ukusanyaji mapato kwani siyo kila chanzo cha
mapato ya Halmashauri kitakusanywa kwa ufanisi kwa kutumia au kwa kutotumia
mawakala.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana mchana (Alhamisi, Juni 30, 2016) wakati akitoa hoja
ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
Alisema
katika ukusanyaji wa mapato, baadhi ya vyanzo vitapaswa kukusanywa na
Halmashauri zenyewe kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Serikali.
“Moja
ya miongozo hiyo ni kwamba kuanzia sasa, iwe kwa kutumia mawakala au
Halmashauri zenyewe ni lazima fedha zinazokusanywa ziwekwe kwenye akaunti ya
Halmashauri na kutumia mifumo ya kielektroniki ili kupunguza au kumaliza kabisa
masuala ya kutumia malipo kwa fedha taslimu (cash transactions),” alisema.
Alisema
katika kutekeleza agizo hilo, Halmashauri itabidi zikubaliane na wakala ni
kiasi gani cha asilimia ya makusanyo kitalipwa kwa wakala na malipo yafanyike
baada ya kukusanya na kuingizwa kwenye akaunti ya Halmashauri.
Alisema
Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura ya 290, inazipa uwezo Mamlaka za
Serikali za Serikali za Mitaa kutoza na kukusanya kodi, ushuru na ada
mbalimbali kama vyanzo vya mapato vya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Sheria
hiyo pia inazipa mamlaka hizo kuteua mawakala wa kukusanya mapato hayo kwa
niaba ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu. Lakini Serikali imebaini changamoto za kiufundi katika kufanya
tathmini ya vyanzo vya mapato; ugumu katika kupata mawakala wenye weledi katika
ukusanyaji mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato, na wakati mwingine
watumishi wenyewe kujipa uwakala kinyume na taratibu zinazomzuia mtumishi
kufanya biashara na taasisi yake,”
alisema.
Alisema
hatua ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia mawakala ni miongoni mwa mikakati
ya kuboresha ukusanyaji mapato na pia kutoa muda mwingi zaidi kwa watumishi wa
mamlaka hizo kushughulika na majukumu ya msingi ya Halmashauri na hasa utoaji
wa huduma kwa wananchi na usimamizi wa miradi ya maendeleo.
“Pamoja
na dhamira nzuri ya hatua hizo, tunayo mifano ya baadhi ya Halmashauri kama
vile Nzega ambayo baadhi ya wahusika wameshinikiza wakitaka zabuni zote wapewe
madiwani. Jambo hili halikubaliki na tena ni kinyume cha maadili ya utumishi,” alisisitiza.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote nchini kwamba kuanzia
Julai Mosi, 2016 zihakikishe zinatumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya
mapato, katika kulipa, kuweka na kutekeleza kikamilifu mikakati madhubuti ya
kuboresha makusanyo iwe yanakusanywa na Halmashauri au na wakala.
Alisema
Mamlaka za Serikali za Mitaa zina wajibu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu
mapato na matumizi ya Serikali pamoja na michango ya wananchi licha ya kuwa
uzoefu unaonesha kuwa mamlaka hizo zina tatizo la kukaa na fedha kwa muda mrefu
kabla ya kuzielekeza kwenye matumizi yaliyokusudiwa.
“Kuchelewesha
kutoa fedha zilizotengwa kwa shughuli zilizopangwa ni kuchelewesha kufikisha
huduma muhimu kwa wananchi. Napenda kuhimiza uzingatiaji wa utaratibu wa kutoa
taarifa kwa wananchi kuhusu mapato na matumizi ya fedha za Serikali katika
ngazi zote ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya umma,” aliongeza.
Mkutano
huo wa tatu wa Bunge ulioanza Aprili 19, 2016 ulikuwa mahsusi kwa ajili ya
kujadili na kupitisha bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Bunge
limeahirishwa hadi Septemba 6, mwaka huu litakapokutana tena mjini Dodoma.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S.L.
P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI,
JUNI 30, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WAZIRI MKUU:SERIKALI ITATOA WARAKA JUU YA UKUSANYAJI MAPATO KUPITIA MAWAKALA.”
Post a Comment