Friday, July 1, 2016
AKUKURU NA TRA WAMTAJA MTU ALIYEKUWA AKIIBIA SERIKALI MILIONI 7 KWA DAKIKA
Do you like this story?
MAMLAKA ya
Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) hatimaye wametaja mfanyabiashara ambaye alibainishwa na Rais
John Magufuli katika hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Ikulu Dar es
Salaam juzi.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,
Valentino Mlowola alimtaja mfanyabiashara huyo kuwa ni Mohammed Mustafa
Yusuf Ali anayetuhumiwa kuiibia Serikali matrilioni ya shilingi kwa kutumia
mashine za kielektroniki (EFDs) ambazo hazijasajiliwa na TRA na kutoa risiti
bandia.
Alisema
TRA kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na uchunguzi ili kubaini makampuni
yote yanayojihusisha na udanganyifu huu, ambapo hadi sasa jumla ya makampuni
manne yamebainika kujihusisha na ukwepaji kodi kwa mtindo huu kuanzia mwaka
2010 hadi 2014; na jumla ya Sh 29,216,900,301.7 imebainika kutokulipwa
serikalini na makampuni hayo kwa kipindi hicho.
Alisema
kwa sasa wanaendelea na mahojiano naye zaidi ili kuwabaini wote wanaohusika na
mfumo huo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Kwa mujibu
wa Kamishna Mkuu wa TRA, Alfayo Kidata aliyeambatana na Mlowola katika mkutano
huo wa waandishi wa habari, makampuni hayo yamekuwa yakinunua risiti za
manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za EFDs ambazo
hazijasajiliwa.
“Makampuni
hayo wakishanunua risiti za manunuzi bandia, hatimaye huzitumia risiti hizo
kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) bila kuwepo na bidhaa au
huduma halisi iliyouzwa au kutolewa na mhusika, kitendo ambacho kinainyima
serikali mapato stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Aliyataja
makampuni hayo kuwa ni pamoja na Skol Building Material Ltd ambayo tangu mwaka
2012 hadi 2013 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 5,464,915,963 na Kodi ya Mapato
yenye thamani ya Sh 10,960,787,861 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 16,425,703,824
kwa kipindi hicho.
Kampuni
nyingine ni Farm Plant (T) Limited ambayo tangu mwaka 2010 hadi 2014 haikulipa
jumla ya VAT ya Sh 5,930,170,573 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh
4,948,393,516 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 10,878,564,089.
Pia imo
kampuni ya A.M.Steel & Iron Mills Limited ambayo kuanzia mwaka 2013 hadi
2014 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 79,016,112 na kodi ya mapato yenye thamani ya
Sh 131,693,518 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 210,709,630.
Kampuni
nyingine ni A.M Trailer Manufacturers Limited ambayo tangu mwaka 2013 hadi 2014
haikulipa VAT ya Sh 638,221,034.80 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh
1,063,701,724. 00 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 1,701,922,758.00.
Alisema
baada ya kubaini ukwepaji kodi huo kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na
uchunguzi wa tuhuma hizo na mara baada ya uchunguzi kukamilika hatua za
kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukwepa kodi.
Alitoa
mwito kwa wafanyabiashara wote kutojihusisha na kununua risiti za bandia na
kudai marejesho ya VAT yasiyostahili kwa kuwa mamlaka imejizatiti kuendelea
kuwabaini wafanyabiashara wanaokwepa kodi na kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria kwa hatua stahiki.
Aidha
alisema uchunguzi wa awali pia umebaini kuwepo makampuni hewa 228 na kusisitiza
kwamba wameusimamisha mfumo huo bandia na kutoa siku tatu kwa kampuni zote
zinazodaiwa kulipa fedha hizo.
“Hakuna
yeyote anayekwepa kodi atasalimika, wote ni lazima walipe na sasa tumedhibiti
mfumo huo bandia,” alisema.
Juzi Magufuli
akizungumza na Ma RC na Ma DC wapya, aliwataka wakasimamie vyema mapato katika
maeneo yao kwani kumekuwepo na baadhi ya watu wajanja wanaotumia vibaya taasisi
za Serikali ikiwemo Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela) TRA kujinufaisha
wenyewe na kuliingizia taifa hasara.
Alisema: “Tulikuwa
tunafuatilia mashine za EFDs zinazokusanya mapato, yupo mtu mmoja alitengeneza
kampuni nyingi zilizokuwa zikimlipa asilimia tano ya VAT na yeye anacheza na
TRA halipi asilimia 18 ya kodi hiyo. Alikuwa anaingiza kati ya shilingi milioni
saba mpaka nane kwa dakika. Serikali ilipoteza matrilioni ya fedha. Huyu mtu
yupo kwenye mikono salama kwa sasa”.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “AKUKURU NA TRA WAMTAJA MTU ALIYEKUWA AKIIBIA SERIKALI MILIONI 7 KWA DAKIKA”
Post a Comment